PENUEL GLORIOUS MINISTRY OF TANZANIA

Wednesday, June 30, 2021

SOMO: SUMU YA SHETANI KWENYE MOYO WA MWANADAMU -1

KITABU CHA SOMO. Matendo 5:3-4.."Petro akasema, Anania, kwa nini Shetani amekujaza moyo wako kumwambia uongo Roho Mtakatifu, na kuzuia kwa siri sehemu ya thamani ya kiwanja? Kilipokuwa kwako, hakikuwa mali yako? Na kilipokuwa kimekwisha kuuzwa, thamani yake haikuwa katika uwezo wako? Ilikuwaje hata ukaweka neno hili moyoni mwako? Hukumwambia uongo mwanadamu, bali Mungu.” Na Askofu Burton Saulo Yuda wa Kanisa la Penuel Mpanda Utangulizi Wakati unataka kujifunza somo hili kuna vitu unapaswa kujiuliza; kwamba ni kweli Shetani anaweza kuujaza sumu moyo wa mtu ? na Je anaweza kuujaza sumu moyo wako wewe? Je ni kweli Shetani anazo sumu za kumjaza mtu? Je Shetani anaujaza moyo mambo gani ambayo ni sumu? Je, vitu hivyo vinavyoitwa sumu vinafaida au hasara? Mwisho wa somo hili moyo uliojaa sumu ili ufe Bwana anaenda kuuganga tena kwa jina la Yesu. MOYO KUJAZWA SUMU NA SHETANI Kabla sijakuelezea ni namna gani Shetani hujaza sumu na kwa njia gani, ngoja nikueleze kidogo kuwa Shetani ni nani. Shetani kwa asili anajulikana kama ni mwizi; huyu anayejaza watu sumu anafanya kazi kuu tatu kwenye maisha ya watu, kwanza ni mwizi. Wakati wowote aonekanapo huja kwa lengo lake la kuiba. Kazi yake ya pili ni kuua yaani aonekanapo popote huja kwa lengo la kuondoa uhai kwenye maisha ya watu na kazi yake ya tatu ni kuharibu, yaani akija kwenye maisha ya mtu huja kwa lengo la kuharibu kila kitu alichonacho. Imeandikwa; Yohana 10:10.. “Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele.” Mahali pengine Shetani anaitwa Mharabu. Sio muharabu yule wa Dubai unayemjua kuwa ni mweupe kwa sura, hapana. Mharabu huyu kwa kiingereza anaitwa Destroyer au mwenye uwezo wa kuharibu. Kwa Kiswahili cha kwaida angeitwa muharibu lakini kwa kiswahili fasaha anaitwa Mharabu na lengo lake ni kuharibu kila kitu masomo kazi, ndoa, biashara n.k. 1 Wakorintho 10:10… “Wala msinung'unike, kama wengine wao walivyonung'unika, wakaharibiwa na mharabu.” Mahali pengine Shetani anajulikana kama muongo na na baba wa uongo. Shetani ni mshawishi wa mambo maovu anashawishi watu hadi wanaharibikiwa. Aliwahi kumshawishi mfalme Daudi kuwahesabu wana wa Israeli kinyume na mapenzi ya Mungu akasababisha Daudi kumkosea Mungu. Shetani akikushawishi unathiriwa moyo na hatimaye unaanza kutenda mambo ambayo si sawa. Shetani mahali pengine anajulikana kama mpanzi wa mambo mabaya kwenye Maisha ya watu. Anaweza kutia vitu vibaya kwa mtu na likakua kama pando baya na hatimaye maisha ya mtu yakaharibika kabisa. Ndio maana Bwana Yesu akasema kila pando lisilopandwa na Baba wa mbinguni litang’olewa kwa sababu Shetani naye hupanda mabaya kwa watu. Shetani anaweza kumtia mtu kifafa, anaweza kutia mtu ujinga, magonjwa n.k. Mathayo 15:13.. “Akajibu, akasema, Kila pando asilolipanda Baba yangu wa mbinguni litang'olewa.” Kwa sababu hiyo Shetani anaweza kuingia kwenye maisha ya mtu kwa makusudi mengi kama nilivyokueleza. Anaweza akaja kama mtu na kusema nawe na kisha kukupandia au kukutia sumu. Shetani anaweza kuongea na mtu na akisha sema naye roho ikamuingia. Kama aliweza kufika kwenye kiti cha enzi cha Mungu na akaanza kusema na Mungu (Ayubu 1:6-7) anaweza pia kumsemesha mtu sumu ikamuingia na mipango ya maisha yake ikaaanza kuharibika. Kwaajili ya kusemeshwa na Shetani ndipo utaona mtu alikuwa na juhudi kwaajili ya mambo ya Mungu gafla anaacha. Neno moja alilolisikia kwa Shetani likaharibu moyo wake na akaanza kuacha mambo yake ya msingi, akaanza kufanya maamuzi mabaya hatimaye anaharibikiwa. Shetani anaweza akaja kama Rafiki lakini kumbe ni yeye katika umbo la kibinadamu ili usijue. Mahali unapoishi mambo yako yameanza kuharibika, upendeleo wako kati yako na Mungu, na watu umepungua sana kwa sababu ya ile sumu iliyokuingia. Yule aliyekusemesha ukabadilika moyo wako ukaacha kumtumikia Mungu, ukaacha huduma, ukamuacha mke wako/ ukamuacha mume wako huyo aliyekusemesha sio mtu hata kama unakaa naye chumba kimoja ni Shetani kwenye mwili wa mtu. Kama vile Mungu akikusemesha roho inakuingia na kukusimamisha vile vile Shetani akikusemesha roho inakuingia na kukuangusha. Unaweza kusemeshwa ukaharibikiwa na kukosa imani juu ya Mungu na ukafanya mambo ya ajabu. Yale maamuzi uliyofanya ukamuacha mke wako/mume wako siku hizi uko single unahaha ni kwaajili ya moyo wako kujazwa sumu. Miaka yote mlikuwa pamoja mkipendana na kuitana kila aina ya majina ya mapenzi imekuwaje leo unampiga, unamtukana? Ni kwa ajili ya sumu ya Shetani. Unakuta mtu ni mlokole kabisa lakini anakuja kwa mwenzake anamwambia uache kusali, unajiuliza ni mtu huyu kweli? Sio mtu ni shetani katika umbo la binadamu. JINSI YA MOYO UNAVYOTIWA SUMU Moyo ni kituo kikuu (centre) cha maisha ya mtu ya kiroho na kimwili. Moyo ndio unabeba mambo yako yote ya kimwili na kiroho. Moyo ndio unawakilisha uhai wa asili wa mtu au ni chemichemi ya uhai wa mtu. Ndani ya moyo ndiko unapata uhai. Ndio maana bibilia ianasema linda sana moyo wako kuliko chochote. Sehemu nyingine moyo unawakilisha uamuzi wako au fikra zako hivyo ni kitu cha msingi kuliko vyote. Mithali 4:23… “Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo; Maana ndiko zitokako chemchemi za uzima.” Mungu anaagiza kwamba moyo wako unapaswa kulindwa kuliko kitu chochote. Kama kungelikuwa na uwezo wa kutumia silaha, basi unapaswa kuchukua bunduki kubwa na kuulinda moyo wako. Anasema linda sana moyo wako kuliko mke wako, kuliko mume wako, kuliko fedha au gari lako. Jiulize mbona wanajeshi hulinda mipaka ya nchi na raia wote, kwanini wewe hulindi moyo wako? Nakukumbusha leo kwa jina la Yesu unapaswa kulinda moyo wako kuliko yote uyalindayo. Shetani akishatia sumu kwa watu, unashangaa mtu anamwambia girl friend wake au boy friend ninakukabidhi moyo wangu? Jinsi gani asivyothamini moyo wake na hatimaye anapata matatizo makubwa. Unamsikia mtu anamwambia mwenzake kaa hapa nikueleze siri zote za moyo wangu, huyu athamini moyo wake kabisa. Bibilia inamtaja Samson kwa kosa lake kueleza siri zote za moyo wake na matokeo yake alitobolewa macho na kuteswa. Unajifunza usipolinda moyo wako kwa kusema kila kitu kilichomo ndani yako utatobolewa macho. Unashangaa magari yanalindwa, mashamba yanalindwa kwa alarm za bei kubwa kwa nini sasa moyo wako hauna ulinzi. Unatakiwa kuweka makombora kulinda moyo wako. Moyo usiokuwa na ulinzi utajazwa sumu na Shetani. Na Shetani akijaza sumu moyo wako hakika utaaribu ndoa yako, utaaribu kazi yako, utaaribu maisha yako na kila kitu chako kitaharibika . Moyo usipolindwa kuna chemchem za sumu zinaanza kuingia ndani yake. Sumu hizi huingia kwa njia nyingi hasa kwa kupitia maneno. Kuna mtu akikusemesha hakika mdomoni mwake inatoka sumu na ikikuingia moyo wako wote unaharibika. Unaweza kuambiwa jambo na mtu gafla ukaanza kumchukia mtu na tabia yako ikaharibika ukawa mtu wa tofauti kabisa, hivyo linda sana moyo kuliko vyote uvilindavyo. Shetani haangaiki sana na pua yako wala miguu, anahangaika na moyo ili pale uzima unapotoka patoke mauti. Unaweza ukawa umeokoka, ukaacha moyo wako bila ulinzi hakika utaharibikiwa. Mtu akisema na wewe angalia sana maneno yake maana yanaweza kuwa sumu kwako. Kuna vitu unafanya kwa hasira, uchungu kwa sababu kuna vitu vimekaa kwenye moyo wako kama sumu, leo Bwana akuponye kwa jina la Yesu. Baada ya Shetani kusema na moyo wa Anania na mkewe, chemichemi za uhai wake zilizima na ndani yake ikaanza kutoka sumu hata kufika hatua kusema uwongo na kumdanganya Roho Mtakatifu. Yeye na mkewe waliunza shamba lao la urithi, lakini kwa sababu shetani alishatia sumu moyoni mwao wakaleta kiasi pungufu cha fungu la kumi. Kwa sababu ya kujazwa sumu na Shetani alifanya jambo lisilo la kawaida na kumdanganya Roho Mtakatifu. Nakutangazia siku ya leo ikiwa umewekewa sumu ndani yako nina iharibu leo kwa jina la Yesu. Matendo ya mitume 5:1-4 “Lakini mtu mmoja jina lake Anania, pamoja na Safira mkewe, aliuza mali, akazuia kwa siri sehemu ya thamani yake, mkewe naye akijua haya, akaleta fungu moja akaliweka miguuni pa mitume. Petro akasema, Anania, kwa nini Shetani amekujaza moyo wako kumwambia uongo Roho Mtakatifu, na kuzuia kwa siri sehemu ya thamani ya kiwanja? Kilipokuwa kwako, hakikuwa mali yako? Na kilipokuwa kimekwisha kuuzwa, thamani yake haikuwa katika uwezo wako? Ilikuwaje hata ukaweka neno hili moyoni mwako? Hukumwambia uongo mwanadamu, bali Mungu.” Shetani akijaza sumu ndani ya mtu kuna mambo yanatokea, mambo hayo ni kama yafuatayo; 1. Kufanya mambo yasiyo ya asili yako Utaona Petro anamwambia Anania, kwanini Shetani ameujaza moyo wako uwongo na kudiriki kumdanganya Roho Mtakatifu. Kila jambo lolote ambalo si la kikawaida chanzo chake ni sumu ya Shetani. Ukiona mwanaume na mwanaume wanaoana fahamu chanzo chake ni sumu ndani ya moyo wao. Sumu ikiingia ndani ya moyo wa mwanadamu ndipo utaona mtu anafanya maamuzi ya hovyo kabisa, anapoteza vitu vya thamani kwa pesa ndogo. Moyo unabadilika anafanya maamuzi ambayo siyo yake mwenyewe

0 comments:

Post a Comment