Wednesday, June 30, 2021
Home »
» SOMO: SUMU YA SHETANI KWENYE MOYO -2
SOMO: SUMU YA SHETANI KWENYE MOYO -2
2. Anabadilika badilika kwenye maamuzi yake
Mtu ambaye ana sumu ya shetani moyo wake unatema mauti badala ya uzima. Wakati Wayahudi wanatafuta namna ya kumuua Yesu,
ndipo shetani akamwingia Yuda na kisha akasema na wakuu wa makuhani akasema nao jinsi ya kumtia mikononi.
Kwa hali ya kawaida mtu hawezi kumuuza baba yake, lakini baada ya kutiwa sumu Yuda alibadilika maamuzi yake na akaenda kujadiliana na wakuu na makuhani namna ya kumtia Yesu hatiani.
Luka 22:3-4.. “Shetani akamwingia Yuda, aitwaye Iskariote, naye ni mmoja wa wale Thenashara. Akaondoka, akaenda akasema na wakuu wa makuhani na majemadari, jinsi atakavyoweza kumtia mikononi mwao.”
Unakuta mtu anawazo zuri sana juu ya maisha yako na anakwambia nitakupa mtaji, nitakupa biashara lakini Shetani akimwingia anabadilika kabisa.
Yuda alikuwa ni mtu mzuri kabisa anatunza fedha za huduma ya Yesu, lakini Shetani alipomuingia andipo akaanza kufanya maamuzi ya kumuuza Yesu.
Yohana 13:2.. “Hata wakati wa chakula cha jioni; naye Ibilisi amekwisha kumtia Yuda, mwana wa Simoni Iskariote, moyo wa kumsaliti;”
Sio kwamba shetani aliweka moyo mwingine ndani ya Yuda bali aliweka sumu kwenye moyo wa Yuda.
Aliweka kitu cha usaliti, yaani uasi, ukawekwa kwenye moyo wa Yuda ndipo sasa akaanza kuwaza kumsaliti.
Sumu ndio hiyo mipango ya usaliti. Ukiona mtu alikuwa na bidii kanisani tena amefika kuitwa Pastor, lakini gafla akaacha hata hasalimii njiani ujue Shetani ameweka sumu ndani ya moyo wake.
Sumu ya Shetani inaharibu tabia za watu, unashangaa watu wawili wanafunga ndoa kanisani na walipooana waakaitana majina yote ya kimapenzi lakini gafla unashangaa mmoja anasema simpendi huyu, simtaki huyu. Ni kwamba Shetani ameweka sumu ndani yake, ikambadilisha moyo na mawazo yake.
Absalomu, mwana wa Daudi, alikuwa na umbu mzuri, jina lake akiitwa Tamari, naye Amnoni, mwana wa Daudi, akampenda. Akamshawishi kwa maneno mengi lakini bada ya kulala naye akamchukia sana.
Unajifunza kwamba unaweza kudanganywa kwa maneno matamu na kaka yule lakini baada ya kubali kulala naye anakuchukia machukio makuu. Wewe binti, usikubali kufanya tendo la ndoa kabla ya ndoa, hata kama unadanganywa kwamba atakuoa usifanye hivyo.
2 Samweli 13:14-15 “Walakini yeye hakukubali kusikiliza sauti yake; naye akiwa na nguvu kuliko yeye, akamtenza nguvu, akalala naye. Kisha Amnoni akamchukia machukio makuu sana; kwa kuwa machukio aliyomchukia yakawa makuu kuliko yale mapenzi aliyokuwa amempenda kwanza. Amnoni akamwambia, Ondoka, nenda zako.”
Linda sana moyo wako kuliko vyote ulivyonavyo, ukiona kijana unafanya tendo la ndoa kabla ya ndoa na anasali kabisa kanisani ujue moyo wake tayari umeharibika.
Miaka ya nyuma mkristo kupata mimba kanisani lilikuwa ni jambo la aibu na kuogopa lakini siku hizi jambo hili limekuwa ni kawaida kabisa.
Bibilia inasema ikimbieni zinaa (1Wakorintho 6:18) lakini utashangaa mtu unashikwa mkono unapelekwa hadi gest, unapelekwa hadi porini lakini bado unasema Shetani mekupitia. Na kwa sababu hiyo utaomba sana, utaimba sana kama huachi hayo huwezi kufanikiwa.
Kuna wakati unaomba lakini macho ya Mungu hayakuoni, wala sikio lake halikusikilizi maombi yako. Ni kwa ajili dhambi zako zinafanya Mungu asikii maombi yako; unaweza kuwa wengi sana na Mungu akasikia kwa mtu mmoja na mwingine asisikie. Ni kwaajili ya moyo uliojaa sumu; Shetani anakujaza uongo hatimaye unafanya makosa na unasema Mungu ni mwenye rehema. Hakika huwezi kufanikiwa.
2 Nyakati 7:14-17 “ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao. Sasa macho yangu yatafumbuka, na masikio yangu yatasikiliza maombi ya watu waombao mahali hapa. Maana sasa nimeichagua nyumba hii na kuitakasa, ili kwamba jina langu lipate kuwako huko milele; yatakuwako na macho yangu, na moyo wangu daima. Nawe, ukienda mbele yangu kama alivyokwenda Daudi baba yako, ufanye sawasawa na yote niliyokuamuru, na kuzishika sheria zangu na hukumu zangu;”
3. Mauti
Ndani ya moyo zikiingia sumu uhai unaondoka. Shetani akijaza sumu vile vitu vinavyoleta uhai ndani yako vinakufa na sumu inajaa ndani yako inakuathiri wewe na watu.
Sumu hii itakufanya kudanganyika na ukidanganyika moyoni na kufanya maamuzi yasiyo sawa hatima yake ni lazima utakufa. Sumu ikiingia ndani yako hata kama upo salama leo siku moja utakufa mambo yako yatakufa, kazi yako itakufa kila kitu chako kitakufa.
Matendo 5:5-11.. “Kilipokuwa kwako, hakikuwa mali yako? Na kilipokuwa kimekwisha kuuzwa, thamani yake haikuwa katika uwezo wako? Ilikuwaje hata ukaweka neno hili moyoni mwako? Hukumwambia uongo mwanadamu, bali Mungu. Anania aliposikia maneno haya akaanguka, akafa. Hofu nyingi ikawapata watu wote walioyasikia haya…. Hata muda wa saa tatu baadaye mkewe akaingia, naye hana habari ya hayo yaliyotokea. Petro akamjibu, Niambie, Mlikiuza kiwanja kwa thamani hiyo? Akasema, Ndiyo, kwa thamani hiyo. Petro akamwambia, Imekuwaje hata mkapatana kumjaribu Roho wa Bwana? Angalia, miguu yao waliomzika mumeo ipo mlangoni, nao watakuchukua nje wewe nawe. Mara akaanguka miguuni pake akafa; wale vijana wakaingia wakamkuta amekufa, wakamchukua nje, wakamzika pamoja na mumewe.”
4. Anafanya vitu ambavyo sio hiari yake
Kuna vitu unafanya sio kwa hiari yako, Shetani anasababisha ufanye si kwa nguvu zako. Shetani akiingia ndani ya moyo anakulazimisha.
Kuna mambo unafanya ingawa ni mabaya lakini unayafanya kwa sababu Shetani ametia sumu kwenye moyo wako na hutendi kama wewe na kwa maamuzi yako, si kwahiari yako.
Warumi 8:19-20 “Kwa maana viumbe vyote pia vinatazamia kwa shauku nyingi kufunuliwa kwa wana wa Mungu. Kwa maana viumbe vyote pia vilitiishwa chini ya ubatili; si kwa hiari yake, ila kwa sababu yake yeye aliyevitiisha katika tumaini”
Ukisikia habari za yule mtu ambaye alikuwa anakaa makaburini, ameacha nyumba yake na ndugu zake na kisha kuamua kuishi makaburini. Alikuwa anakimbizwa hadi jangwani kwa nguvu za pepo. Ndipo sasa unaona mtu anakimbia mume, anakimbia mke, anakimbia biashara kwa nguvu za pepo.
Luka 8:29.. “Kwa kuwa amemwamuru yule pepo mchafu amtoke mtu yule. Maana amepagawa naye mara nyingi, hata alilindwa kifungoni na kufungwa minyororo na pingu; akavikata vile vifungo, akakimbizwa jangwani kwa nguvu za yule pepo.”
Watu wengi wamefeli masomo, wameshindwa kazi, wameacha ndoa ukimuuliza anasema nimesikia moyo wangu unasema, nimesikia roho mtakatifu anasema na mimi. Huyo sio roho mtakatifu ni roho mtakafujo. Roho mtakatifu hawezi kukutenga na watu, hawezi kuvunja ndoa yako.
Unahitaji moyo wako uwe salama siku zote kwa maana moyo ukijaa sumu fikra zako zina haribika. Ndipo unaona mtu alikuwa anamsifia sana mume wake lakini gafla sasa anamchukia sana kuliko chochote, hawezi kuizuia wala kuitawala nafsi yake.
Hawezi kuizuia nafsi yake, unamwambia mtu kabisa tabia hii ni mbaya uiache lakini hawezi kuacha kwa sababu hawezi kujizuia; moyo wake umejazwa sumu.
1Timotheo 5:6.. “Bali, yeye asiyejizuia nafsi yake amekufa ingawa yu hai.”
Ukiona umekuwa mgumu sana na utoaji kanisani ujue moyo wako umejazwa sumu, ni sawa na vile Anania na mke walipatana kumdanganya Roho Mtakatifu.
Sio wewe ufanyae bali sheria ya dhambi ikaayo ndani yako, yale mambo unayapenda huwezi kuyafanya lakini yale ambayo hutaki kuyatenda ndio unayatenda. Ndani ya moyo wako umejazwa na mambo ya mabaya; ndio maana unawaza na kutenda mabaya. Leo Bwana akuponye kwa jina la Yesu.
Moyo ukipata madhara, yale unayoatenda si wewe bali ile sumu ikaayo ndani ya moyo wako; kuna maamuzi umefanya ambayo sio sawa, ni ya maamuzi yaliyoathirika na sumu ya Shetani.
Moyo wako ukihuishwa na uahi ukabaki ndani yako utafanya yale mazuri, hakuna atayakulazimisha kwenda kanisani, hakuna atakayekulazimisha kutoa kwajili ya Bwana utajikuta unafanya mwenye kwa kupenda.
0 comments:
Post a Comment