Jambo la Pili : Neema moja inaweza kukusaidia kuomba na kupata Neema zingine.
Angalia kwenye Biblia;
Kutoka 33:13 …Basi, sasa nakuomba, ikiwa nimepata neema mbele zako, unionyeshe njia zako, nipate kukujua, ili nipate neema mbele zako; ukakumbuke ya kuwa taifa hilo ndilo watu wako.
Musa alipokuwa anafanya maombi alisema kuwa, kama amepata Neema mbele za Mungu, 'apate neema mbele zake'. Ukisoma hiyo sentensi ina neno 'neema' mara mbili;
yaani kuna 'neema' mbili tofauti zinazungumziwa kwenye mstari mmoja.
Neema ya kwanza anayoitaja ni Neema ambayo inamsaidia kwenye kuomba vitu vingine. Ni msingi wa maombi yake, kwa sababu haanzi kuomba kwanza mpaka ameuliza kama ana Neema za kusongea mbele za Mungu ili kufanya maombi ya vitu vingine.
Neema ya pili inayotajwa kwenye mstari ni ombi. Anaomba apate neema. Na ili apate hii neema ya pili lazima awe na neema ya kwanza aliyoitaja. Asipopata neema ya kwanza maana yake na Neema ya pili ataikosa. Neema ya pili ni ombi la yeye kutaka Mungu awe pamoja naye ili kuwaongoza wana wa Israel kuelekea Kanaani.
Kwa hiyo neema moja inaweza kukusaidia kuomba neema nyingine.
Si wengi sana wanaojua kuwa neema zipo nyingi. Kuna neema nyingi sana lakini ufunguo wa neema zote tunazopokea ni Yesu Kristo, maana ndiye aliyekuja na Neema na kweli (Yoh 1:17). Kwahiyo Neema ya kwanza inayoweza kukusaidia kuombea neema zingine ni Neema ya kuwa na Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wa maisha yako.
Ndani yake yeye (Yesu) ndimo tunachota kila aina ya Neema, na ndio maana tunasema tupo kwenye kipindi cha neema na siyo kipindi cha sheria kama ilivyokuwa kwenye Agano la kale. Msingi wa Agano jipya ni neema.
Yohana 1:16 …Kwa kuwa katika utimilifu wake {Yesu} sisi sote tulipokea, na neema juu ya neema.
Biblia ipo wazi, inasema katika utimilifu wake Yesu Kristo (alitimilika msalabani) tulipokea na neema juu ya neema.
Kupitia msalaba wa Yesu kristo siyo tu kwamba tunapata neema, bali tunapata na neema juu ya neema . Maana yake kupitia msalaba unaweza ukapata neema nyingi tu. Neema ya kumwamini Yesu Kristo na kuamini alichokifanya msalabani ni mlango wa wewe kupokea neema zingine nyingi.
Nachotaka uone pia ni kwamba neema siyo moja, zipo neema nyingi sana ambazo ziliachiliwa msalabani ni kazi yetu sisi kuzichukua.
Ndiyo maana kwenye Biblia anasema 'tulipokea na neema juu ya neema'. Anatumia neno 'tulipokea' na siyo tutapokea. Anatumia wakati uliopita na siyo uliopo. Maana yake neema zilishakuja kupitia msalaba, siyo zitakuja, bali zilikuja! Ni swala la sisi tu kuzichukua msalabani tu.
2 Wakorintho 9:8 ….Na Mungu aweza kuwajaza kila neema kwa wingi, ili ninyi, mkiwa na riziki za kila namna siku zote, mpate kuzidi sana katika kila tendo jema;
Matendo ya Mitume 4:33 …Na mitume wakatoa ushuhuda wa kufufuka kwake Yesu kwa nguvu nyingi, na neema nyingi ikawa juu yao wote
Ukisoma kwenye hiyo mistari utagundua kitu kwamba Neema zipo nyingi na wala haipo moja.
Tupo kwenye kipindi cha Neema kwa sababu tupo kwenye kipindi cha kupitia utimilifu wa Yesu msalabani tulipokea Neema nyingi.
Wakorintho inatwambia kwamba Mungu aweza kuwajaza kila Neema kwa wingi, Neno 'kila' linaonyesha kwamba zipo nyingi lakini Mungu anaweza kukujaza zote.
Kama Mungu anaweza kutupa kila Neema basi na tupige magoti kwake atupe Neema / za kutosha.
Kuna neema ya kumjua Mungu ;kuna neema ya kumtumikia Mungu ; kuna Neema ya kushiriki ibada, n.k Omba Mungu akupe Neema nyingi ili uwe kwenye kipindi cha neema kweli kweli, kuliko unatamba kwa watu kwamba upo kwenye kipindi cha Neema kumbe hata nini maana ya Neema hujui.
Jambo la 3: Neema yako inaweza kuwabeba na watu wengine.
Neema ipo kwa ajili ya kutufanya tuishi ndani ya kusudi la Mungu. Na kusudi la Mungu ni kwa ajili ya watu wa Mungu. Kwa hiyo unaweza ukapewa Neema wewe ila ikawasaidia na wengine!
Angalia kwenye Biblia;
1 Petro 4:10 …kila mmoja kwa kadiri alivyoipokea karama, itumieni kwa kuhudumiana; kama mawakili wema wa neema mbalimbali za Mungu.
Biblia inatuonyesha kuwa kama mawakili wa Neema inatubidi tuwe tunahudumiana kwa kadiri ya karama ya kila mmoja wetu.
Ni kama anataka kutwambia kwamba Neema uliyopata iliyokupa hiyo Karama itumie kwa ajili ya kuwahudumia wengine , Maana ukirudi kwenye jambo la kwanza
nilikwambia kuwa NEEMA ya Mungu ndiyo inaonyesha kusudi/ huduma/ Karama ya Mungu kwenye maisha yako.
Ukipokea neema ya Mungu itumie kuhudumia watu.
Kutoka 33:16 ..Kwa maana itajulikanaje kuwa nimepata neema mbele zako, mimi na watu wako? Siyo kwa sababu unakwenda pamoja nasi, hata mimi na watu wako tutengwe na watu wote walio juu ya uso wa nchi?
Musa aliomba Neema yeye pekee yake kwenye mstari wa 13. Kwenye mstari wa 16 anataka kujua kama Neema aliyoomba itawasaidia na wenzake? Maana yake Musa alijua kabisa kwamba akipata Neema yeye itawasaidia na watu wengine pia.
Mwanzo 6:8 …Lakini Nuhu akapata neema machoni pa BWANA.
Wasomaji wa Biblia wanajua kwamba Neema aliyoipokea Nuhu haikumsaidia yeye pekee yake, bali iliokoa uhai wa mbegu ya viumbe hai duniani na uhai wa watu nane, yaani Nuhu, hamu, yafethi na Shemu pamoja na wake zao; lakini hao saba hawakupata Neema isipokuwa Nuhu pekee yake, na kwa sababu hiyo wengine wote saba waliokolewa kwa faida ya Neema iliyokuwa kwa Nuhu.
Ukipata Neema tambua kuwa ni kwa ajili ya watu pia. Mungu atusaidie.
Jambo la 4: Unaweza ukawa na Neema ya Mungu lakini isijae.
Neema ya Mungu ina kipimo chake, inaweza kujaa au kutokujaa. Sasa unaweza ukawa una Neema ya Mungu lakini ikawa haijajaa katika kiwango kinachotakiwa.
Ngoja tuangalie kwenye Biblia alafu uone kitu huko.
Matendo ya Mitume 6:8 ..Na Stefano, akijaa neema na uwezo, alikuwa akifanya maajabu na ishara kubwa katika watu.
Biblia inamtaja stefano kama mtu aliyejaa Neema. Kama Biblia imemtaja stefano kuwa alijaa Neema maana yake walikuwepo watu wengine ambao hawakujaa Neema, japokuwa walikuwa nayo.
Je wewe umejaa Neema ya Mungu? Imani yako katika kristo ndiyo itaamua neema iweje ndani yako.
Waebrania 12:15 …mkiangalia sana mtu asiipungukie neema ya Mungu; shina la uchungu lisije likachipuka na kuwasumbua, na watu wengi wakatiwa unajisi kwa hilo.
Waebrania inatwambia kuwa mtu asiipungukie neema ya Mungu. Na anatoa ni tahadhari maana anaanza kwa kusema, mkiangalia sana, mtu asiipungukie neema ya Mungu; ni tahadhari hii.
Kwa hiyo kama mtu hataangalia sana [ kama hatachukua tahadhari ] anaweza kujikuta ameipungukia neema ya Mungu kwa kujua au kwa kutokujua.
Imani yako thabiti juu ya Yesu Kristo na kile alichokifanya msalabani basi ndiyo itakufanya uendelee kuwa na neema ya Mungu yote. Ukiugeuzia mgongo msalaba na Neema ya Mungu inaanza kupungua kwako. Tunapokea Neema kwa njia ya msalaba kupitia Yesu Kristo.
Msisitizo upo kwenye kutambua kuwa inawezekana unaishi ukiwa na Neema ya Mungu lakini ikiwa ni ndogo sana; chukua tahadhari.
INAENDELEA SEHEMU YA TATU






