Kitabu cha somo : 1 Tim 2:1-2….. Basi, kabla ya mambo yote, nataka dua, na sala, na maombezi, na shukrani, zifanyike kwa ajili ya watu wote; kwa ajili ya wafalme na wote wenye mamlaka, tuishi maisha ya utulivu na amani, katika utauwa wote na ustahivu.
Watu wanapofanya kitu kwa pamoja wanahitaji viongozi. Na kila mara uongozi unafuatana na kiasi fulani cha mamlaka. Karibu kila siku tunasikia habari za watu wanaotumia mamlaka vibaya. Wanasiasa wengine na viongozi wa makampuni makubwa wanajipatia faida kwa njia ambazo hata mtu mwenye dhamiri ilioharibika kabisa ataona si za haki. Na tukisema ukweli hata ndani ya madhehebu na makanisa yetu inatokea ya kwamba watu wanatumia vyeo vyao vibaya. Hayo yote yanaweza kuwafanya watu wengi kudharau na kukataa aina zote za uongozi. Mwisho wake tunapata jumuiya ambamo kila mtu anapigana na mwenzake. Jumuiya ya namna ile haiwezi kudumu muda mrefu. Lakini Biblia inatuonyesha kiongozi aina nyingine ambaye ni kama chumvi katika dunia hii inayoendelea kuharibika.
Mungu
huwaweka viongozi kwa sababu zifuatazo :-
- Mamlaka yote yanatoka kwa Mungu
- Viongozi wa Agano la Kale waliwekwa na Mungu
- Viongozi wa Agano Jipya waliwekwa na Mungu
- Viongozi watatoa hesabu mbele za Mungu
Ni muhimu kiongozi yeyote yule asitawale bila kutoa hesabu ya kazi yake. Viongozi wasiowajibika popote pale watatumia mamlaka yao kwa faida yao wenyewe na kuwakandamiza watu wengine. Ndiyo maana nchi nyingi zinatumia njia ya demokrasia kuwachagua viongozi. Hivyo kwa njia ya uchaguzi watu wanapata nafasi kuwanyang'anya viongozi wao cheo wakitumia mamlaka vibaya. Mfumo huu unasaidia kwa sehemu, lakini pia umewafanya viongozi wengine kuwa wajanja wa kuficha ukweli wa mambo ili waendelee kutawala. Kutoa hesabu mbele ya watu inaonekana hakutoshi kuwafanya viongozi watafute yalio mema kwa ajili ya watu walioko chini yao.
Biblia kama ilivyo kawaida yake ina namna bora ya kutatua tatizo hili. Katika somo hili tutajaribu kuchora picha ya kiongozi bora katika mfumo wa kibiblia. Uongozi wa kibiblia hasa unahitajika katika kanisa, lakini pia unafaa sana katika biashara, jamii, na siasa. Kwanza tuone jambo la mamlaka ya wanadamu linavyofanya kazi katika mipango ya Mungu.
Rum
13:1-7 ; Yn 19:10-11 ; 1 Pet 2:11-17
Watawala na viongozi wamechukua madaraka kwa kupitia mbinu nyingi tofauti katika historia ya binadamu, na wameondolewa madarakani kwa njia nyingi tofauti. Lakini Paulo anatuambia hata hivyo anayewapa viongozi mamlaka ni Mungu mwenyewe. Yesu alimwambia Pilato "Wewe hungekuwa na mamlaka yo yote juu yangu, kama usingepewa kutoka juu". Na Petro anawataja mfalme na wakubwa kwamba wemetumwa na Mungu. Watawala waliotajwa hapa tunajua kutoka historia ya kwamba walikuwa ni watawala wabaya waliopenda rushwa na kuwakandamiza watu. Walifanana na watawala wengi katika dunia ya leo. Yaani hata viongozi hao waovu walipata mamlaka yao kutoka kwa Mungu. Aliwaruhusu kutawala, angalau kwa muda. Mipango ya Mungu inapita fahamu zetu mara nyingi, lakini huenda anafanya hivyo viongozi wazuri wanapokosekana kabisa. Heri kuwa na viongozi wabaya kuliko dunia yote ikose utaratibu. Si ajabu wakipatikana watu wenye uwezo na nia nzuri Mungu anawapandisha na kuwaondoa viongozi walioharibika. Lakini ya muhimu kujua ni kwamba mamlaka yote yanatoka kwa Mungu.
Hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu. Zaidi ya yote Mungu
anaangalia sana nani ataongoza watu wake wateule. Katika Agano la Kale kuna
mifano mingi inayoonyesha alivyoingilia moja kwa moja uchaguzi wa viongozi wa
Israeli. Alilwapa wana wa Israeli waamuzi, wafalme, makuhani na manabii.
Amu 6:1-40 ; 1 Sam 16:1-13 ;Eze 2:3
Amu 6:1-40 ; 1 Sam 16:1-13 ;Eze 2:3
Viongozi wa taifa walipoongoza kufuatana na mapenzi ya Mungu nchi yote ilisitawi na kubarikiwa kwa njia nyingi. Walipomsahau Mungu shida na dhiki zilianza. Manabii walikuwa wajumbe wa Mungu wa kuwaonya watawala walipofanya makosa, na kuwatia moyo walipokata tamaa. Bila viongozi hawa waliochguliwa na Mungu bila shaka taifa la Israeli lingelipoteza urithi wake wote wa kiroho. Kwa vile Mungu aliingilia kati, utirhi huo mpaka leo upo kwa faida ya yeyote anayeamini.
Mungu anaonyesha upendo ule ule kwa
watu wake katika Agano Jipya kama alivyowaonyesha watu wa Israeli katika Agano
la Kale. Hata leo anawaita viongozi wenye jukumu la kuongoza kanisa lake.
Ef 4:11 ; 1 Kor 12:27-31 ; Gal 1:15 ;Rum 1:5
Viongozi wa kiroho wa kufaa hawachaguliwi tu kufuatana na
elimu yao au vipawa vyao vya kimwili vya kuongoza watu au kwa vile wengi
kanisani wanawapenda. Lazima tutafute mapenzi ya Mungu tunapochagua viongozi
mbalimbali kanisani. Mungu anajali sana nani anaongoza watu wake. Kiongozi
anayechaguliwa kwa misingi isiyo sahihi anaweza kuzuia mipango ya Mungu mahali
pale anapoishi na kufanya kazi. Hapo kuna hatari ya kwamba inambidi Mungu
kumwondoa kiongozi yule madarakani kwa njia ambayo haitampendeza mtu yeyote.
Karne zilizopita watawala wa nchi za Ulaya walidai kwamba
wamewekwa na Mungu. Kwa hiyo walifikiri wanaweza kutawala walivyopenda wenyewe
bila kujali mahitaji ya wananchi. Lakini walisahau kwamba ikiwa Mungu
aliwaweka, yeye pia siku moja atadai watoe hesabu ya kazi walioifanya. Maana
katika Rum 13.1-7 tunasoma kwamba watawala waliwekwa ili wayaadhibu matendo
mabaya na kuyasifu matendo mazuri. Wakitumia mamlaka yao kwa kufanya mambo
mengine watahukumiwa na Mungu.
Kama Mungu ndiye anayewapa viongozi mamlaka ina maana ya kwamba kila kiongozi atajibu mbele za Mungu jinsi alivyoongoza. Huu ni ukweli hata kama kuna vyombo vya kukagua kazi kama vile bodi, kamati za uongozi, na uchaguzi wa kitaifa. Mungu bado anaweza kumwondoa yeyote asieongoza kwa kumtii Mungu. Kadiri wajibu unavyoongezeka ndivyo kiongozi atakavyodaiwa zaidi.
Kama Mungu ndiye anayewapa viongozi mamlaka ina maana ya kwamba kila kiongozi atajibu mbele za Mungu jinsi alivyoongoza. Huu ni ukweli hata kama kuna vyombo vya kukagua kazi kama vile bodi, kamati za uongozi, na uchaguzi wa kitaifa. Mungu bado anaweza kumwondoa yeyote asieongoza kwa kumtii Mungu. Kadiri wajibu unavyoongezeka ndivyo kiongozi atakavyodaiwa zaidi.
Lk 12:48 , 1 Kor 3:13 , 2 Kor 10 ; Ebr 13:7 ; Rum 14:12
Kiongozi anayefahamu kwamba atatoa hesabu kwa Mungu anahakikisha kwamba mwenendo wake unapatana na Neno la Mungu. Hata kama kiongozi ameelewa kwa sehemu tu yalioandikwa katika Biblia ujuzi huo utafanya tofauti kubwa katika uongozi wake. Hapo tayari kutakuwa na kipimo kingine muhimu zaidi kuliko ya kwamba wachaguzi, bodi au kanisa waufurahie uongozi wake. Na haongozi tena ili ajipendeze mwenyewe tu. Haya yanamhusu kiongozi yeyote kama ni wa kanisa, kampuni, shirika au serekali.
HITIMISHO
Mamlaka yote yametoka kwa Mungu. Mungu anaweza kumwondoa yeyote madarakani wakati wowote. Anajali hasa nani anongoza watu wake. Aliingilia mara kwa mara kuwachagulia watu wa Israeli viongozi wao. Hata leo anawaita viongozi waongoze kanisa lake. Viongozi wote wa aina yoyote watatoa hesabu mbele za Mungu walivyotumia madaraka yao.
0 comments:
Post a Comment