PENUEL GLORIOUS MINISTRY OF TANZANIA

PGMT

ASKOFU WA KANISA LA PENUELI MAKAO MAKUU MPANDA KATAVI

Thursday, December 21, 2017

SOMO: KIONGOZI BORA WA KIROHO [KIKRISTO]



KITABU CHA SOMO: Mwanzo 12: 1-2…Bwana akamwambia Abramu, toka wewe katika nchi yako ,na jamaa zako ,na nyumba ya baba yako ,uende mpaka nchi nitakayokuomyesha .Nami nitakufanya wewe kuwa Taifa kubwa ,na kukubariki na kulikuza jina lako ;  nawe uwe baraka.

Na: Askofu Burton Saulo Yuda wa kanisa la Penueli [ T ]

1.   UTANGULIZI.
Popote unapoona kazi ya Mungu imesonga mbele na kufanya vizuri lazima kuna kiongozi aliyesimama kwenye nafasi yake vizuri.

Imekuwa ni tabia ya Mungu mara zote kumchagua mtu ili kuyafanikisha malengo na mipango yake.

Mfano:
a)   Mungu alimuandaa Ibrahimu na kumwita ili kuanzisha Taifa
b)  Akamwandaa Yusufu ili kulihifadhi Taifa hilo Mwanzo 45: 3 - 9, 50: 20 - 21.
c)   Akamwandaa Musa ili kulitoa Taifa hilo Utumwani - Kut.3:2-14.
d)  Akamwandaa Joshua kuliongoza Taifa hilo kuteka nyara, kupigana vita na kuliingiza Kanani - Yoshu 1: 1 - 9.
e)   Mungu alitumia wanaume na wanawake katika kufikia malengo yake kama vile Nabii Debora - Amuzi 4:4, Esta 7: 3 - 6 n.k.
f)    Pia Mungu aliwaongoza na kuwaelekeza waamuzi na wafalme katika kulisimamia kundi lake (watu) la Mungu, pia aliwatumia Manabii ili kuwaonya na kuwasahihisha watu wa Mungu;
g)  Na hatimaye alimtuma mwanaye wa pekee mpendwa Yesu Kristo kuja kufa na kufufuka kwa ajili ya kuukomboa ulimwengu kutoka katika utumwa wa dhambi - Yoh. 3:16, Math. 1:21.
h)  Yesu naye alipoondoka akamtuma Roho Mtakatifu ili atuongoze salama - Yoh. 14: 16,26, Rumi. 8:14

Jambo la pekee katika ufalme wa Mungu, mtu mmoja anaweza akaleta/akasababisha ushindi mkuu katika kanisa au Huduma.

Hii ni ajabu Mungu anasema katika Ezek. 22:30 “Nami nikatafuta mtu miongoni mwao, atakaye tengeneza boma, na kusimama mbele zangu mahali palipobomoka, kwa ajili ya nchi, nisije nikaiharibu, lakini sikuona mtu.”

Kumbuka:
Hitaji kubwa la nyakati zote tangu vizazi na vizazi, katika watu wa kada zote, jamaa, Taifa, Mataifa, Taasisi na Mashirika ya dini ni kupata viongozi wenye sifa na uwezo wa kuwaongoza wengine,

pia wenye uwezo na hekima katika kuwaunganisha watu ili kuwafanya kuwa wamoja katika kutumia karama, vipawa, talanta, huduma na rasilimali walizonazo kwa manufaa ya maendeleo yao. Pia waweze kufikia na kukamilisha jambo/malengo na mipango yao waliyokusudia.

Viongozi wanajua wanalopaswa kulifanya na wana uwezo


2.   MAANA YA UONGOZI.
Marko.10:45, 1Petr.2:21, Yoh.10:10 – 11
Uongozi ni hali/tendo la kuongoza.
Ni hali ya kutangulia mbele, kusimamia, kulinda na kuelekeza watu njia au mwelekeo wa kuuendea au kufikia malengo Fulani. na kuwachukua watu mbele zaidi ya pale walipo sasa .1Tim.4;11 - 12, 1Petr.2:21.
Kiongozi ni mtu Yule ajuaye njia na yale apaswayo kupita nayo na kuzingatia katika njia hiyo.

Ni mtu Yule ajuaye mwelekeo wa jambo hilo au malengo hayo na anauwezo wa kuwatangulia na kuwavutia (kushawishi) wengine wamfuate.

Ni mtu aliyepewa dhamana (aliyeaminiwa) na Mungu kuongoza watu wengine (kuwatumikia). Mfano: Yesu - Yoh.14:6; 10:2 - 4, Paulo - 1Kor.11:1; 4:16.

Ni mtumishi (mtumwa) wa wale anaowaongoza.
Mfano: Musa - Kut.10:25 - 26; 13:21 - 22, Yuda - Mw.46:28
                                                                                
Kumbuka:

Kiongozi wa Kiroho siyo mtawala (boss) bali ni mtumishi (mtumwa).

Kiongozi ni kielelezo (mfano) wa kuigwa na, kufuatwa na wengine – Mfano Unaosimama mbele yao kuwaongoza.


Hivyo maisha ya kiongozi lazima yawe kielelezo katika maeneo makuu matano:-
A.   Katika Usemi: Chunga (angalia) sana matumizi ya ulimi (yale uyasemayo). Yakobo 3:1 - 12.

B.   Katika Mwenendo: (Tabia) - Maisha yako ya kila siku machoni pa watu. Math.5:16, 1Petr.2:11 - 12, Fil.2:14- 16.

C.   Katika Upendo: Kujitoa, kujali, kuhudumia na kuhurumia. Yoh.3:16, Math.9:35 - 38.

D.  Katika Imani: Maisha ya kumtegemea Mungu. Ebr.10:38; 11:1,6, Hesabu.14:11, Yer.17:5 - 8, Rumi.1:17, Gal3:11.

E.  Katika Usafi: Maisha Matakatifu - yenye ushuhuda mzuri mbele za watu. Zaburi.16:3, Kumb.23:14, 1Kor.3:16 - 17, 1Petr.1:16.

Somo litaendelea wiki ijayo .....

Tuesday, November 14, 2017

UJASIRIAMARI


SOMO :AINA YA WATEJA AMBAO UNATAKIWA KUWAEPUKA MAPEMA KWENYE BIASHARA YAKO

Katika biashara ni kawaida kukutana na wateja wa aina tofauti tofauti na wateja wote kama tujuavyo ni muhimu na hutakiwi kumpa huduma yako mteja vibaya hadi ajisikie kwamba hataweza tena kuja kwenye biashara yako.

Mteja anatakiwa kujaliwa na kupewa huduma ambayo itamfanya ajione kwamba yeye ni mfalme kwa mazingira yoyote yale uliyo. Naamini hilo linawezekana sana kwako na unatakiwa kulifanya hilo katika uhai wote wa biashara yako.

Pamoja na kwamba mteja anatakiwa kujaliwa hivyo na ni muhimu, lakini, wapo aina ya wateja ambao inatakiwa kuwa nao makini sana katika biashara yako ili wateja hawa wasije wakaleta matatizo mengine kwenye biashara yako.

Wateja hawa ni wateja gani? Twende pamoja kujifunza;-

1. Wateja wanaolalamika sana.

Wapo wateja ambao kazi yao ni kulalamika sana. Wateja hawa wanalalamikia kitu hiki au kile kwenye biashara na kushindwa kuongea ukweli na kutatua changamoto za pamoja. Wateja hawa ni hatari sana kwenye biashara yako.

Wateja hawa ni moja ya wateja unaotakiwa kuwaepuka sana. Ni rahisi kukuharibia biashara yako na kusababisha wateja wengine wakukimbie kwa sababu ya kulalamika sana kusiko na msingi. Wateja wapya watafikiri kweli bidhaa zako ni mbovu kumbe la.

2. Wateja wanaokupotezea muda sana.
Pia wapo wateja ambao naweza kusema wao ni kama wana nia  ya kukupotezea muda wako. Wateja hao si ajabu ukakuta wanauliza kitu fulani kwa muda mrefu sana na wanakiangalia na kukichunguza hata bila ya kununua pengine.

Unachotakiwa kuwa makini nacho hapa ni kuwa makini na wateja wa namna hii unapokutana nao ana kwa ana na hata wale unaokutana nao kwenye mitandao. Fanya hivi bila wao kujua kwamba unawaepuka.

3. Wateja wanaojiona wao ni maalumu sana.
                                                   
Kuna wateja ambao wanapenda kujiona wao ni muhimu sana kuliko wateja wengine. Wateja hao ni rahisi tu kudai namba ya meneja wako au bosi wako ili wamweleze kile wanachokitaka wao wenyewe.

Kwa kifupi unapokuwa na wateja hawa nao ni wasumbufu sana na wanapenda kufanya kila wanachokitaka kwenye biashara yako ilimradi tu waonekane. Hivyo unatakiwa kuwa makini nao na kujua pia jinsi ya kuwakabili ii wasilete matatizo mengine.

4. Wateja wanaotaka kupatanisha kila kitu.

Sina shaka unawajua wateja ambao ukiwatajia bei ya kitu, wao ni kutaka kupatanisha na kuomba punguzo kila wakati. Unapokuwa na wateja wa namna hii wengi basi biashara yako itakuwa na usumbufu sana.

Vipo vitu ambavyo havihitaji kupatanishwa, bei na kila kitu kinaeleweka, sasa unapokuwa na mteja anayetaka kila kitu kiwekwe kwenye mapatano hapa unatakiwa pia uwe makini sana, vinginevyo utafanya biashara kwenye mazingira magumu.

Hawa ndio wateja ambao unatakuiwa kuwaepuka au kuwa nao makini sana kwenye biashara yako. Sijasema wateja hawa uwafukuze au uwajibu vibaya, ila unatakiwa kuwa nao makini ili wasije wakakuvurugia wateja wengine ambao ulitakiwa kuwa nao kwenye biashara.

Monday, November 6, 2017

SOMO: NGUVU YA MUNGU NDANI YA KANISA.




Kitabu cha somo: , 2 Wakorintho 2 :4…., Wakorintho 4:20
Na. Mch. Kiongozi Burton saulo Yuda wa kanisa la PGMT Mpanda

NGUVU ni uweza au mamlaka ya kufanya jambo Fulani,
                       
 sisi kama wakristo tunahitaji nguvu ya kutuwezesha kutenda mapenziya Mungu   na kazi za Mungu duniani, na Biblia inasema hatuwezi kutenda , kwa usahihi duniani kama hatuta kuwa na nguvu za Mungu,

unapoongelea ukristo mahali jua unaongelea nguvu kwa maana ukristo ni nguvu.
                                                                         
Injili ya Yesu kristo imejengwa katika nguvu za MUNGU. Tofauti kati ya ukristo na dini nyingine ni nguvu iliyo ndani ya jina la Yesu..

Kama tulivyoona ukristo sio maneno matupu tu au tunavyokili bali ukristo umejengwa kwenye nguvu ya Mungu.. nguvu ya kuponya, kufufua, kufungua na kuokoa..

 na ndio maana mtume Paulo anasema kwenye kitabu cha Wathethalonike 1:8.. kuhubiri kwetu hakukuwa katika maneno bali katika Nguvu ya Mungu..

 1 Timotheo 1:7.. ´´Mungu hakutupa roho ya hofu bali roho ya nguvu´´

 na ndio maana biblia inasema kuwa ´´nanyi mtapokea nguvu akishawajilia juu yenu Roho Mtakatifu´´

Yesu yu hai, na ana nguvu, Yesu wetu hayupo kaburini, alifufuka ..hayupo ndani ya tumbo la bikira Maria bali yupo hai mbinguni na anatenda kazi duniani..

 Waefeso 3:20.. ´´ kulingana na NGUVU itendayo kazi ndani yetu´´ ndani ya kila mtu aliyeokoka kuna nguvu ya Mungu..

Waefeso 6:10 ´´katika uweza..¨ uweza unamaanisha nguvu.. YESU ALITUPA NGUVU HIZO ambazo twazipata kupitia vyanzo viwili..

NGUVU YA MSALABA WA YESU KRISTO..

Unaweza kujiuliza kwanini ukiweka msalaba wa Yesu kwenye nchi kama Iran, au nchi nyingi za kiarabu utapingwa sana na unaweza hata kuuawa, Hii ni kwasababu msalaba wa Yesu kristo una nguvu.. kuna nguvu ipatikanayo kwenye msalaba inaitwa ¨NGUVU YA MSALABA¨
                      
 1 Wakorintho 1:18 ¨ujumbe wa msalaba kwao wanaopotea ni upuuzi lakini kwetu sisi tunaoamini ni nguvu ya Mungu¨ kumbe kwenye msalaba wa Yesu Kristo kuna uweza uletao wokovu. Msalaba wa Kristo una nguvu.

Kwanini ujumbe wa msalaba unabeba nguvu?,

Unaweza kujiuliza ni kwanini, iwe nguvu ya msalaba na isiwe nguvu ya kitu kingine kama jua, mwezi, dunia au nabii..

, tunaweza kuona kuwa maneno saba ya mwisho ya Yesu Kristo kabla ya kufa ni maneno ya muhimu na nguvu ya msalaba imejengwa kwenye maneno yale.. ni muhimu kujua Yesu alipigwa kwa ajili Yetu.. na magonjwa na matatizo yetu yalipigwa pamoja naye.


MANENO 7 ALIYOYASEMA YESU KABLA YA KUFA..


i.) Mathayo 27:46, Kwa wakati ule alibeba dhambi zetu zote. Na ndio maana Mungu akamwacha pale msalabani tunajua kuwa Mungu alimwacha kwa maneno ambayo Yesu alitamka akisema ´´ baba mbona umeniacha´´ baada ya Yesu kubeba d

hambi za ulimwengu, Mungu akamwacha na Yesu akasurubishwa kwa dhambi ambazo hakutenda bali alitenda.. Yesu alisulubiwa kwa makosa YETU..


ii.) Luka 23: 34 -Katikati ya maumivu Yesu alisamehe.. watu wa dunia wanaweza kukwambia nimekusamehe lakini sitasahau lakini Yesu akiwa msalabani na katikati ya maumivu makuu ya msalaba akasema ´´baba wasamehe maana hawajui walitendalo´´

 ZABURI 103:3 Nguvu ya msalaba unatupa nguvu ya kusamehe, kuna watu wengi wapo kwenye matatizo kwasababu ya kuto kusamehe.. ni kanuni ya Mungu kusamehe na kuponya

. tunajifunza hili kwa wale waliomleta mtu kwa Yesu , mgonjwa akiwa kwenye godolo.. na Yesu kabla ya kumponya alimtangazia msamaha wa dhambi kwanza na baada ya hapo akamponya.. Kumbe msalaba unatuwezesha kusamehewa..


iii.) Luka 23:42-43 - ¨..Leo utakuwa pamoja nami peponi ..¨ hili ni neno ambalo Yesu alimwambia mmoja kati ya wale wanyang´anyi, akimwambia kuwa tutakuwa wote peponi,

Yesu alisurubiwa pamoja na wanang´anyi.. kumbe usitishwe na mtu anaye vaa msalaba akasema ni mtu wa Mungu, kwasababu wengine wanaweza kuvaa msalaba wa wanyang´anyi..

 na kwa andiko hili tunajifunza kuwa nguvu ya msalaba inatupa nguvu ya kukumbukwa kwenye Ufalme wa Yesu.. kumbe msalaba unatupa nguvu ya kukumbukwa ..

Mungu anakumbuka maombi yako, kazi yako, maisha yako na hata taifa lako.. Mtu yeyote awezi kukuhakikishia kwenda na kuuona ufalme wa Yesu isipokuwa msalaba wa Yesu ndio unaotupa uwakika wa kuuona Ufalme wa Mungu ´´hakuna jina jingine duniani, litupasalo kuokolewa kwalo isipokuwa jina la Yesu..


iv.)Luka 23:46, Kwa mtu yeyote aliyeokoka ,amekabidhiwa kwenye mikono ya Yesu kristo.. na hutakufa mpaka siku ya Bwana , kwasababu roho yako imekabidhiwa kwenye mikono ya Yesu Kristo.. huu ni ulinzi ambao kila mtu aliyeokoka anakuwa nao.. tupo mikononi mwa Mungu na hakuna mtu awezaye kututoa kutoka katika mikono ya Yesu Kristo..


v.) Yohana 19:29 Yesu akiwa msalabani , alikuwa anajali mahusiano.. hii inaonyesha kuwa msalaba wa Yesu unatupa usalama ndani ya mahusiano na wazazi na watu wengine.. Msalaba wa Yesu unatupa mahusihano bora . ukimwomba Mungu akupe nguvu ya mahusiano.. Kumbe msalaba ulileta Nguvu ya upatanisho.. Nguvu ya msalaba inaleta watu pamoja , watumishi wa Mungu pamoja, familia pamoja.. ujumbe wa msalaba ni upuuzi kwao wasioamini lakini kwetu sisi ni NGUVU YA UPATANISHO.


vi.) Yohana 19:28 ¨..ninasikia kiu..¨ hapa Yesu alikuwa amekaa msalabani kwa muda , na alisikia kiu.. kwa kuwa hakuwa amekunywa maji.. kumbe msalaba wa Yesu unakupa kiu ya kumtafuta Mungu, kiu ya kuomba, kiu ya kuponya na kuokoa na rahisi kusikia watu wakisema nyinyi watu wa ufufuo na uzima kwanini kila kitu mnataka mtende nyinyi.. ni muhimu kujua kuwa msalaba wa kristo unatupa kiu ya kutenda na kuthibitisha nguvu ya Mungu.. na inawezeka ulipokuwa umeokoka ulipata hamu sana ya kuomba na kumtafuta Mungu..lakini baada ya muda ile kiu imepotea basi kama unatatizo hilo ni wakati wa kwenda mbele ya msalaba wa Yesu kristo.. na kuomba KIU ya kumtafuta Mungu na Mungu atakupa

vii.) Yohana 19:30 ´´.. Yesu alipopokea kile kinywaji akasema IMEKWISHA´´ Kimsingi hakuna aliyemuua Yesu bali aliutoa uhai wake , ili aupokee tena.. na kimsingi Yesu alitenda mambo makubwa ya ufalme wa Mungu, na kwasababu hiyo shetani akakusanya watawala na watu wamuue Yesu na alipokuwa msalabani na kupiga kelele kusema imekwisha.. shetani akafikiri kuwa amemuangamiza na inawezekana kabisa kule kuzimu mashetani walianza kushangilia na inawezekana hata wachawi wa kipindi kile walienda kwenye sherehe .. lakini katikati ya sherehe yao. na Yesu akiwa nanig´inia msalabani Yesu akasema IMEKWISHA..

Baada ya Yesu kusema kuwa IMEKWISHA.. BIBLIA inasema

I. Dunia ikatikisika,.. kumbe Nguvu ya msalaba inaweza kutikisa dunia,
II. Makaburi yakafunguka, miili mingi ya watakatifu wengi ikafufuka. Kumbe Nguvu ya msalaba yaweza kurudisha. Na ndio maana mimi nashangaa watu wanaokataa kuwa wafu hawafufuki..najiuliza ni msalaba gani wanao uhubiri.. labda ni misalaba ya wale wanyang´anyi ..
III. Miamba ikavunjika kumbe msalaba wa Yesu unaweza kuvunja miamba.
IV. Jua likatiwa giza
V. Pazia la hekalu likapasuka.


KWELI KADHAA KUHUSU NGUVU YA MSALABA..


Kipindi cha zamani kulikuwa na aina za usulubishaji.. aina ya kwanza ni ya mti mmoja kama namba moja, ya pili ilikuwa alama ya kuzidisha yaani ´X´ , tatu ni wa alama ya T, na alama ya kujumlisha nah ii inamaanisha msalaba wa Yesu unatupa kujumlisha , kuongezeka, na kukua.. sisi tumesulubishwa pamoja na kristo

Yesu alisurubishwa kwenye mlima, na mahali pale kila mtu aliweza kumuona ,, watu kutoka kila mahali walimuona.. kumbe Yesu alisurubiwa mlimani ili kila mtu aone nakama Yesu alivyoinuliwa mlimani ili kila mtu amuone..´´kama vile Musa alivyomuinua nyoka jangwani mwana wa adamu naye aliinuliwa..

Na unagundua watu walimuona Yesu akisurubiwa mbele ya watu, njiani, mlimani na alipo taka kupaa akaenda mlimani pia..ili watu wote wamuone,, kumbe kama ulikuwa chini na watu walikuona chini Msalaba wa Yesu utakuinua mbele ya watu wote walikuona ukiahibika..

Yesu akashuka kuzimu katika zile siku tatu alipokuwa amekufa, akamnyang´anya funguo za mamlaka.. na hapo akamkanyaga kichwa shetani .. kutimiza andiko ´´uzao wa mwanamke utamkanyaga nyoka kichwa´´



NGUVU YA KABURI LA KRISTO LILILO WAZI..

Hii ni nguvu tunayoipata kutoka katika nguvu ya kaburi la kristo.. kwa maana malaika alikuja kaburini na kukuta .. walinzi pale na baada kutetemesha lile eneo .. wakalisukuma jiwe la kaburi na kulikalia na hapo Yesu akafufuka na kutoka kaburini.. nah ii ni nguvu ya ufufuo na baada ya siku chache kabla ya kupaa akatangaza ´´mamlaka yote nimewapa ninyi ..´´ tuna mamlaka ya kuitawala dunia.. Nguvu ya kaburi lililowazi imetupa mamlaka.. sisi tuko ndani ya Yesu na Yesu yupo ndani yetu.. ´´tunalindwa na NGUVU za Mungu kwa njia ya imani..

KIONGOZI BORA - 1





Kitabu cha somo : 1 Tim 2:1-2….. Basi, kabla ya mambo yote, nataka dua, na sala, na maombezi, na shukrani, zifanyike kwa ajili ya watu wote; kwa ajili ya wafalme na wote wenye mamlaka, tuishi maisha ya utulivu na amani, katika utauwa wote na ustahivu.


Watu wanapofanya kitu kwa pamoja wanahitaji viongozi. Na kila mara uongozi unafuatana na kiasi fulani cha mamlaka. Karibu kila siku tunasikia habari za watu wanaotumia mamlaka vibaya. Wanasiasa wengine na viongozi wa makampuni makubwa wanajipatia faida kwa njia ambazo hata mtu mwenye dhamiri ilioharibika kabisa ataona si za haki. Na tukisema ukweli hata ndani ya madhehebu na makanisa yetu inatokea ya kwamba watu wanatumia vyeo vyao vibaya.  Hayo yote yanaweza kuwafanya watu wengi kudharau na kukataa aina zote za uongozi. Mwisho wake tunapata jumuiya ambamo kila mtu anapigana na mwenzake. Jumuiya ya namna ile haiwezi kudumu muda mrefu. Lakini Biblia inatuonyesha kiongozi aina nyingine ambaye ni kama chumvi katika dunia hii inayoendelea kuharibika.

Mungu huwaweka viongozi kwa sababu zifuatazo :-
  1. Mamlaka yote yanatoka kwa Mungu
  2. Viongozi wa Agano la Kale waliwekwa na Mungu
  3. Viongozi wa Agano Jipya waliwekwa na Mungu
  4. Viongozi watatoa hesabu mbele za Mungu


Ni muhimu kiongozi yeyote yule asitawale bila kutoa hesabu ya kazi yake. Viongozi wasiowajibika popote pale watatumia mamlaka yao kwa faida yao wenyewe na kuwakandamiza watu wengine. Ndiyo maana nchi nyingi zinatumia njia ya demokrasia kuwachagua viongozi. Hivyo kwa njia ya uchaguzi watu wanapata nafasi kuwanyang'anya viongozi wao cheo wakitumia mamlaka vibaya. Mfumo huu unasaidia kwa sehemu, lakini pia umewafanya viongozi wengine kuwa wajanja wa kuficha ukweli wa mambo ili waendelee kutawala. Kutoa hesabu mbele ya watu inaonekana hakutoshi kuwafanya viongozi watafute yalio mema kwa ajili ya watu walioko chini yao.

Biblia kama ilivyo kawaida yake ina namna bora ya kutatua tatizo hili. Katika somo hili tutajaribu kuchora picha ya kiongozi bora katika mfumo wa kibiblia. Uongozi wa kibiblia hasa unahitajika katika kanisa, lakini pia unafaa sana katika biashara, jamii, na siasa. Kwanza tuone jambo la mamlaka ya wanadamu linavyofanya kazi katika mipango ya Mungu.

Mamlaka yote yanatoka kwa Mungu
Rum 13:1-7  ; Yn 19:10-11  ; 1 Pet 2:11-17 

Watawala na viongozi wamechukua madaraka kwa kupitia mbinu nyingi tofauti katika historia ya binadamu, na wameondolewa madarakani kwa njia nyingi tofauti. Lakini Paulo anatuambia hata hivyo anayewapa viongozi mamlaka ni Mungu mwenyewe. Yesu alimwambia Pilato "Wewe hungekuwa na mamlaka yo yote juu yangu, kama usingepewa kutoka juu". Na Petro anawataja mfalme na wakubwa kwamba wemetumwa na Mungu. Watawala waliotajwa hapa tunajua kutoka historia ya kwamba walikuwa ni watawala wabaya waliopenda rushwa na kuwakandamiza watu. Walifanana na watawala wengi katika dunia ya leo. Yaani hata viongozi hao waovu walipata mamlaka yao kutoka kwa Mungu. Aliwaruhusu kutawala, angalau kwa muda. Mipango ya Mungu inapita fahamu zetu mara nyingi, lakini huenda anafanya hivyo viongozi wazuri wanapokosekana kabisa. Heri kuwa na viongozi wabaya kuliko dunia yote ikose utaratibu. Si ajabu wakipatikana watu wenye uwezo na nia nzuri Mungu anawapandisha na kuwaondoa viongozi walioharibika. Lakini ya muhimu kujua ni kwamba mamlaka yote yanatoka kwa Mungu.

Viongozi wa Agano la Kale waliwekwa na Mungu
Hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu. Zaidi ya yote Mungu anaangalia sana nani ataongoza watu wake wateule. Katika Agano la Kale kuna mifano mingi inayoonyesha alivyoingilia moja kwa moja uchaguzi wa viongozi wa Israeli. Alilwapa wana wa Israeli waamuzi, wafalme, makuhani na manabii.

Amu 6:1-40 ; 1 Sam 16:1-13 ;Eze 2:3 

Viongozi wa taifa walipoongoza kufuatana na mapenzi ya Mungu nchi yote ilisitawi na kubarikiwa kwa njia nyingi. Walipomsahau Mungu shida na dhiki zilianza. Manabii walikuwa wajumbe wa Mungu wa kuwaonya watawala walipofanya makosa, na kuwatia moyo walipokata tamaa. Bila viongozi hawa waliochguliwa na Mungu bila shaka taifa la Israeli lingelipoteza urithi wake wote wa kiroho. Kwa vile Mungu aliingilia kati, utirhi huo mpaka leo upo kwa faida ya yeyote anayeamini.

Viongozi wa Agano Jipya waliwekwa na Mungu
Mungu anaonyesha upendo ule ule kwa watu wake katika Agano Jipya kama alivyowaonyesha watu wa Israeli katika Agano la Kale. Hata leo anawaita viongozi wenye jukumu la kuongoza kanisa lake.
Ef 4:11 ; 1 Kor 12:27-31  ; Gal 1:15  ;Rum 1:5
Viongozi wa kiroho wa kufaa hawachaguliwi tu kufuatana na elimu yao au vipawa vyao vya kimwili vya kuongoza watu au kwa vile wengi kanisani wanawapenda. Lazima tutafute mapenzi ya Mungu tunapochagua viongozi mbalimbali kanisani. Mungu anajali sana nani anaongoza watu wake. Kiongozi anayechaguliwa kwa misingi isiyo sahihi anaweza kuzuia mipango ya Mungu mahali pale anapoishi na kufanya kazi. Hapo kuna hatari ya kwamba inambidi Mungu kumwondoa kiongozi yule madarakani kwa njia ambayo haitampendeza mtu yeyote.

Viongozi watatoa hesabu mbele za Mungu
Karne zilizopita watawala wa nchi za Ulaya walidai kwamba wamewekwa na Mungu. Kwa hiyo walifikiri wanaweza kutawala walivyopenda wenyewe bila kujali mahitaji ya wananchi. Lakini walisahau kwamba ikiwa Mungu aliwaweka, yeye pia siku moja atadai watoe hesabu ya kazi walioifanya. Maana katika Rum 13.1-7 tunasoma kwamba watawala waliwekwa ili wayaadhibu matendo mabaya na kuyasifu matendo mazuri. Wakitumia mamlaka yao kwa kufanya mambo mengine watahukumiwa na Mungu.

Kama Mungu ndiye anayewapa viongozi mamlaka ina maana ya kwamba kila kiongozi atajibu mbele za Mungu jinsi alivyoongoza. Huu ni ukweli hata kama kuna vyombo vya kukagua kazi kama vile bodi, kamati za uongozi, na uchaguzi wa kitaifa. Mungu bado anaweza kumwondoa yeyote asieongoza kwa kumtii Mungu. Kadiri wajibu unavyoongezeka ndivyo kiongozi atakavyodaiwa zaidi.
Lk 12:48  , 1 Kor 3:13 , 2 Kor 10  ; Ebr 13:7 ; Rum 14:12

Kiongozi anayefahamu kwamba atatoa hesabu kwa Mungu anahakikisha kwamba mwenendo wake unapatana na Neno la Mungu. Hata kama kiongozi ameelewa kwa sehemu tu yalioandikwa katika Biblia ujuzi huo utafanya tofauti kubwa katika uongozi wake. Hapo tayari kutakuwa na kipimo kingine muhimu zaidi kuliko ya kwamba wachaguzi, bodi au kanisa waufurahie uongozi wake. Na haongozi tena ili ajipendeze mwenyewe tu. Haya yanamhusu kiongozi yeyote kama ni wa kanisa, kampuni, shirika au serekali.

HITIMISHO

Mamlaka yote yametoka kwa Mungu.  Mungu anaweza kumwondoa yeyote madarakani wakati wowote. Anajali hasa nani anongoza watu wake. Aliingilia mara kwa mara kuwachagulia watu wa Israeli viongozi wao. Hata leo anawaita viongozi waongoze kanisa lake. Viongozi wote wa aina yoyote watatoa hesabu mbele za Mungu walivyotumia madaraka yao.