KITABU CHA SOMO:1 Kor 6:17-18 '' Kwa hiyo, Tokeni kati yao, Mkatengwe nao, asema BWANA, Msiguse kitu kilicho kichafu, Nami nitawakaribisha. Nitakuwa BABA kwenu, Nanyi mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wa kike,''
Maandiko hayo ni sehemu tu ndogo ya maandiko yanayolitambulisha Kanisa la KRISTO duniani.
Kanisa hai wametengwa na uovu wa dhambi na wametengwa na mambo ya kidunia yaliyo machukizo(Machafu).
Ndio maana huwezi kumuona Askofu akiwa disko akicheza.Huwezi kumuona Mkristo aliyeokoka akiwa kwa mganga wa kienyeji.Huwezi kumuona Mchungaji anatoa talaka.
Huwezi kumuona Mteule wa MUNGU akivuta sigara wala bangi na tena huwezi kumuona mteule wa KRISTO akitumia madawa ya kulevya.Huwezi kuona kanisa wakichukua mapanga na mikuki wakienda kulipiza kisasi kwa maadui zao.
Kanisa ndilo pekee linalosababisha amani Duniani.Kanisa ni la muhimu sana duniani.Siku Kanisa la MUNGU likiondolewa duniani ndipo neema itatoweka.
Kibiblia katika migao saba ya nyakati huu ni wakati wa Kanisa au wakati wa Neema.Kanisa la KRISTO ndilo pekee linalomwabudu MUNGU aliye hai na wa kweli.Kama kuna kanisa halijafikia hali hiyo basi hilo sio kanisa la KRISTO ila ni kanisa la kibinadamu tu.Katika Kanisa MUNGU ameweka viongozi na wasimamizi ili kazi ya MUNGU itendeke vizuri.
Matendo 20:28 '' Jitunzeni nafsi zenu, na lile kundi(Kanisa) lote nalo, ambalo ROHO MTAKATIFU amewaweka ninyi kuwa waangalizi ndani yake, mpate kulilisha kanisa lake MUNGU, alilolinunua kwa damu yake mwenyewe.''
Kanisa ni la Muhimu sana ndio maana shetani huliwinda kanisa kuliko kitu chochote. Lakini kanisa linamshinda shetani kwa damu ya YESU KRISTO na kwa Neno la ushuhuda na kwa kuvumilia katika MUNGU aliye hai.
Ufunuo 12:11 ''Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa.''
Kwa sababu kanisa ndicho kitu pekee ambacho shetani hakitaki basi amejribu mara kadhaa kuleta makanisa feki yanayomtukuza yeye na mengine yanamwabudu yeye, lakini hiyo haina maana kwamba kanisa la kweli halipo bali lipo na linazidi kuchanua.
shetani amejaribu kubuni dini nyingi sana lakini Kanisa la MUNGU lipo na litaendelea kuwepo na litaendelea kushinda na zaidi ya kushinda maana kanisa la KRISTO ndilo lililolibeba kusudi la MUNGU.
Madhehebu sio kanisa ila ni ni sehemu tu ambapo kanisa(Wakristo) wanakutana na kumwabudu MUNGU. Ndio maana wakati mwingine dhehebu moja linaweza kuhama kutoka kwa KRISTO kwa sababu ya viongozi wao waliojikinai lakini Kanisa la kweli la KRISTO bado lipo na linaendelea.
Hatuendi mbinguni kama dhehebu bali tutaenda mbinguni kama kanisa la KRISTO lililoshinda duniani.Kiongozi wa Kanisa akinaswa na shetani hakika kondoo kutawanywa kiroho itakuwa rahisi sana.
Mara nyingine tumesikia baadhi ya viongozi wa kanisa la kweli wakivamiwa na shetani na kuondoka katika kusudi la MUNGU.
Hapa nimekuandalia mambo saba ambayo mimi ninaona kama ndiyo yanayoweza kulitafuna kanisa la kweli.
1.Dhambi kwa viongozi wa kanisa.
Hosea 4:6 '' Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa; kwa kuwa wewe umeyakataa maarifa, mimi nami nitakukataa wewe, usiwe kuhani kwangu mimi; kwa kuwa umeisahau sheria ya Mungu wako, mimi nami nitawasahau watoto wako.''
Madhara makubwa zaidi yanayoweza kuliathiri kanisa ni dhambi kwa viongozi wa kanisa. Watu wa kanisani wanaweza wakaangamizwa sawasawa na watu wa mataifa kwa sababu ya viongozi wa kanisa. Kiongozi wa kanisa akiisahau sheria (Neno la MUNGU lote) anaweza kusababisha matatizo makubwa ya kiroho kwa kanisa.
Kiongozi akiwa mdhambi itakuwa vigumu sana yeye kukemea dhambi katika kanisa na kwa njia hiyo watu wa MUNGU watakuwa wanaangamiza kwa kukosa maarifa.Kama mchungaji ni mzinzi ni vigumu sana yeye kukemea uzinzi.Kama Mchungaji ni mwizi ni vigumu sana kukemea wizi.
Kama Askofu ni muongo ni vigumu sana kukemea uongo kanisani.
2.Viongozi wa kanisa kutendea kazi kila neno wanaloambiwa na waumini au jirani wa waumini.
1 Timotheo 5:19-22 ''Usikubali mashitaka juu ya mzee, ila kwa vinywa vya mashahidi wawili au watatu. Wale wadumuo kutenda dhambi uwakemee mbele ya wote, ili na wengine waogope. Nakuagiza mbele za Mungu, na mbele za Kristo Yesu, na mbele za malaika wateule, uyatende hayo pasipo kuhukumu kwa haraka; usifanye neno lo lote kwa upendeleo. Usimwekee mtu mikono kwa haraka, wala usizishiriki dhambi za watu wengine. Ujilinde nafsi yako uwe safi.''
Katika maandiko haya tunaweza kujifunza mambo mengi sana lakini kulingana na somo langu katika kipengele hiki cha pili, kunahitajika umakini sana kwa viongozi wa kanisa katika vile wanavyoambiwa na waumini au majirani wa baadhi ya waumini.
Kwanza kiongozi anapoambiwa jambo na mmoja wa waumini wake ambalo linamweka hatiani mtu mwingine haitakiwi kiongozi huyo kumwita haraka haraka tu mtuhumiwa na kumuonya au kumtenga, mambo hayo yanalitafuna sana kanisa leo.
Haina maana kwamba usifanyie kazi unayoambiwa na waumini wako au majirani wa waumini wako lakini hakikisha unafanya uchunguzi wa kina wewe mwenyewe ili pasitokee uonevu.
Kama kuna mtu umemuonea wewe mchungaji hakika mtu huyo hata kama atakuwa anakuja kanisani lakini hatakusikiliza na hatazingatia Neno la MUNGU unalomfundisha, hadi uweke mambo sawa.
Mara nyingine watu wenye makosa ndio huwa wa kwanza kukimbilia kwa Mchungaji ili kuwasema wengine kama njia ya kujisafisha na kuonekana wema.
Inawezekama mmoja wa wana kanisa anatuhumiwa na mtu mwingine wa kanisani kwamba ni mzinzi kwa sababu tu alionekana akitembea barabarani saa saba usiku.
Mchungaji kama atamwita mtuhumiwa haraka tu na kumfukuza kanisani au kumsema hadharani kanisani, na kama jambo hilo amesingiziwa hakika hapo kanisa litakuwa limetafunwa sana maana huyo naye anaweza akaanza kuitafuta haki yake kwa nguvu, anaweza akaacha kwenda kanisani na kujiangamiza kabisa, anaweza akarudi nyuma kiroho.
Kama amekosea inabidi kiongozi ajilidhishe kwanza ndipo atoe hukumu. Namna nzuri ya kujilidhisha ni kupata ushahidi kutoka kwa watu wawili au watatu ndivyo Biblia inashauri hapo juu.
Dhambi lazima zikemewe kanisani lakini iwe ni kweli dhambi imetendeka, sio kusingiziwa.Biblia inakushauri kiongozi wa kanisa kwamba usihukumu kwa haraka ila thibitisha kwanza. Usipendelee mtu, lakini kama utaamua haraka haraka tu mambo yanayowahusu waumini hakika unaweza kujikuta umependelea pasipo sababu.
3.Kuwepo wakala wa shetani katikati ya kanisa.
1 Yohana 4:1-3 ''Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na MUNGU; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani. Katika hili mwamjua ROHO wa MUNGU; kila roho ikiriyo kwamba YESU KRISTO amekuja katika mwili yatokana na MUNGU. Na kila roho isiyomkiri YESU haitokani na MUNGU. Na hii ndiyo roho ya mpinga Kristo ambayo mmesikia kwamba yaja; na sasa imekwisha kuwako duniani.''
Shetani hutaka sana kuingia kanisani ili aharibu utakatifu wa kanisa.
Kanisa ni lazima lisimame katika kweli ya Neno la MUNGU.
Viongozi wa kanisa ni lazima sana walisimamie kusudi la MUNGU kwa kulitii sana Neno la MUNGU.Kwa tamaa za pesa kuna baadhi ya watumishi hutunga vitu vya uongo ili tu kujipatia waumini au kupata pesa.
Sio kila miujiza ni ya MUNGU na sio kila anyehubiri watu ni anataka watu hao waende uzima wa milele. Kila mtu anaweza kuwa mchungaji akiamua lakini kama huyo hamtii KRISTO hakika huyo ni wakala wa shetani kanisani.roho ya mpinga Kristo ipo na kazi yake ni kuaondoa watu kwa KRISTO.
Hatuhitaji kumwabudu MUNGU kupitia sanamu au maji ya baraka, hatutakiwi kumwabudu MUNGU kupitia watu wanaojiita MUNGU.Tunatakiwa kumwabudu MUNGU kupitia YESU KRISTO na sio vinginevyo.
4. Kanisa kuacha maombi.
1 Thesalonike 5:17 '' ombeni bila kukoma; ''
Maombi ni maisha hivyo hayatakiwi kuwa ya msimu tu bali ya siku zote.
Kanisa likisahau maombi kuna madhara yatatokea maana kuona rohoni kutapungua, hamu ya kuendelea na wokovu itapungua.
Kanisa lisipokuwa na maombi ni rahisi shetani kupanda magugu ndani ya kanisa na kuyang'oa magugu hayo ikawa ni vigumu.Kanisa halitakuwa na maombi tu bali pia ni lazima kanisa liwe na maombi ya kufunga kila mara.
Kanisa kama mtu binafsi wa kanisani lazima afundishwa kuomba na kufunga na awe anafunga ili kunoa makali yake ya kiroho na ili aweze kujibiwa mahitaji yake anayoyataka.Kuna mengine hayawezi kuondoka katika kanisa hadi kanisa lifunge na kuomba.
Mathayo 17:21 ''Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga.''
5. Kanisa kutembea katika maono ya uongo yanayoambatana na ujanja ujanja wa watumishi.
Mathayo 15:8-9 ''Watu hawa huniheshimu kwa midomo; Ila mioyo yao iko mbali nami. Nao waniabudu bure, Wakifundisha mafundisho Yaliyo maagizo ya wanadamu.''
Kama kanisa litamwacha KRISTO na Neno lake hakika shetani atachukua nafasi tu na jambo hilo kupelekea uongo kuanza kuliendesha kanisa.
shetani akitawala kanisa ni lazima waumini wawekewe mipaka na kufundishwa kujiona kwamba wao tu ndio kanisa na kwingine kote ni kwa shetani.
Biblia ndio inatakiwa iwe ushahidi na sio watumishi kuwadanganya watu.
Sio kila mchungaji au Askofu ameitwa na MUNGU, Wengine wamejita na wengine wameitwa na shetani.
Shetani ni baba wa uongo hivyo na watumishi wake lazima wabuni vitu vya uongo na lazima kanisa litembee katika maono ya uongo, mambo haya yanalitafuna kanisa sana.
Leo kuna wachungaji hawamhubiri KRISTO tena bali wanajihubiri wenyewe na kudanganya watu.
Kanuni ya Biblia pia inatafasiriwa vibaya na baadhi ya watu. Ngoja nikuambie; Japokuwa Ibrahimu Ni Baba Wa Imani Lakini Hiyo Haina Maana Kwamba Sara Ni Mama Wa Imani.
Mambo Ya Kiroho Huwa Tofauti Na Mambo Ya Kibinadamu. Tukiruhusu Kanisa Liifuate Dunia Basi Ipo Siku Tutasikia Kwamba Stephano Au Ayubu Ni Babu Wa Imani.
Dunia Leo Imeingia Kanisani Ndio Maana Kuna Mawakala Wa shetani Hujipachika Katika Baadhi Ya Maandiko Na Kudai Maandiko Hayo Yaliwatabiri Wao. Kuna Watu Hudai Wao Ni Eliya Amerudi Duniani, Kuna Watu Hujiita Kristo, Kuna Watu Hujiita Henoko Aliyerudi Duniani, Wengine Hudhani Kuna Mtu Anaitwa Mama Wa Mungu leo.
Kuna Watu Hujiita Mungu Muumbaji Aliyekuja Kuishi Na Wanadamu Na Kuna Waongo Original Hudai Biblia Iliondolewa Zamani Na Kuja Kitabu Kingine.
Kanuni Ya Biblia Iko Tofauti Sana Na Kanuni Za Kibinadamu Au Kanuni Za Kimwili.
Ukitaka Biblia Ikufuate Utaishia Pabaya. Wewe Mwanadamu Ndio Unatakiwa Uifuate Biblia. Biblia Haiwezi Kubadilishwa Na Mazingira Wala Haiwezi Kubadilishwa Na Wanadamu. Kataa Kuokoka Harafu Utarajie Mbingu, hakika hakuna mbingu kwa wanaokataa kuokolewa na BWANA YESU
(Yohana 3:16-21). Mkatae YESU Ukidhani Utafika Mbinguni, hakika huwezi kufika(Matendo 4:12)
6. Kanisa kukosa upendo.
1 Petro 1:22-23 ''Mkiisha kujitakasa roho zenu kwa kuitii kweli, hata kuufikilia upendano wa ndugu usio na unafiki, basi jitahidini kupendana kwa moyo. Kwa kuwa mmezaliwa mara ya pili; si kwa mbegu iharibikayo, bali kwa ile isiyoharibika; kwa neno la Mungu lenye uzima, lidumulo hata milele. ''
Upendo wa KiMUNGU ni hali ya kumpenda mtu bila kujali mtu huyo alivyo au ana sifa gani.Lazima kanisa liwe na upendo. Kanisa lazima limpende
mchungaji wao na sio kumsema vibaya.
Kumbuka kuwa mkimsema vibaya mchungaji wenu hakuna atakayemsema vizuri huko nje, hakuna atakayekuja kuokoka maana atadhani kanisa halifai kumbe ni kukosekana kwa upendo.
Lazima kanisa wapendane wote bila kujali cheo cha mtu au hadhi ya mtu. Ukikosekana upendo wa KIMUNGU kanisani hakika jambo hilo litalitafuna sana kanisa na kanisa halitastawi kamwe.
1 Kor 13:4-7 ..''Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni; haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya; haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli; huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote.-
7. Kutokubali kukosolewa au kusahihishwa.
1 Kor 8:2 ''Mtu akidhani ya kuwa anajua neno, hajui neno lo lote bado, kama impasavyo kujua.''
Hakuna mwanadamu anayejua yote na hakuna mwanadamu anayeweza yote.Katika kanisa wote tunategemeana.
Hata Mchungaji kuna baadhi ya mambo hajui na anahitaji kusaidiwa, Hata mama mchungaji sio kwamba anajua yote kuliko wanawake wote kanisani.
Sio kwamba wazee wa kanisa hawana la kusaidiwa bali yapo tena mengi.
Sio kwamba matumizi ya kanisa yakienda vibaya basi wanaotaka kushauri wafukuzwe kanisani.
Vitu vya kanisa ni vya kanisa na sio mali ya kiongozi wa kanisa hivyo kuna wengine akitaka kusaidiwa tu kwa upole anaanza kuhubiri kwamba roho ya uasi na kukosa heshima imeingia kanisani.
Kama Mchungaji angekuwa anajua yote ana anaweza yote basi kusingekuwepo kiongozi wa ibada kanisani, kusingekuwepo mashemasi kanisani, kusingekuwepo wapiga vyombo na kusingekuwepo waimbaji. Lakini kwa sababu kila mtu kanisani ni muhimu basi ni muhimu sana kusaidiana ili kuondoa lawama zisizokuwa na sababu.
MUNGU AKUBARIKI SANA
Tuesday, July 6, 2021
HATUA ZA KUMSAIDIA KIJANA ALIYEOKOKA AISHI MAISHA YENYE USHUHUDA MZURI
Mtume Paulo katika waraka wake kwa Timotheo anamwambia hivi, ‘Mtu awaye yote ASIUDHARAU ujana wako, bali uwe KIELELEZO kwao waaminio, katika usemi na mwenendo, na katika upendo na imani na usafi. JITUNZE nafsi yako, na mafundisho yako. DUMU katika mambo hayo; maana kwa kufanya hivyo UTAJIOKOA NAFSI YAKO NA WALE WAKUSIKIAO PIA’ (1Timotheo 4:12 & 14).
Sentensi hizi zinatuonyesha kwamba kijana yeyote ambaye amefanya uamuzi wa kuokoka, kwa hakika amefanya maamuzi ambayo yanamtaka amaanishe katika kumfuata kwake Yesu au kuuishi wakovu wake. Pamoja na kumpa Yesu maisha yake ni lazima kijana afanye maamuzi ya kuishi maisha ya kudumu kumpendeza Mungu kwa kuzikubali gharama zinazohusiana na wokovu aliouchagua na si kuishi maisha yenye kupelekea jina la BWANA kutukanwa kama ilivyo kwa baadhi ya vijana wengi leo.
Ukisoma mstari huu wa 1Timotheo 4:14 kwenye toleo la kiingereza la ESV unasema ‘Keep a close watch on yourself and on the teaching. Persist in this, for by so doing you will save both yourself and your hearers’. Kwa mujibu wa dictionary ya kigiriki na kiebrania neno ‘save’ lina maana ya kuweka huru (deliver), kulinda (protect), kuponya (heal), kutunza (preserve), kuokoa (save). Jambo muhimu ambalo Mtume Paulo alikuwa akilisisitiza hapa ni hili; jambo muhimu si tu kumpokea Yesu kama Bwana na mwokozi wako, bali kila mwamini ana kazi kubwa ya kufanya ili KUULINDA NA KUUTUNZA WOKOVU WAKE.
Moja ya changamoto kubwa sana ambazo zinawakabili vijana wengi waliokoka leo ni kuipenda dunia. Kuipenda dunia kumekuwa tanzi kwa vijana wengi na kwa sababu ya kuipenda dunia; (a) Mahusiano ya vijana wengi na Mungu wao yameharibika (b) Maisha ya vijana wengi yamekosa uelekeo (c) Kutokana na uovu wao jina la Bwana Yesu limekuwa likitukanwa.
Katika kile kitabu cha 1Yohana 2:16 ni dhahiri kwamba dunia imejaa TAMAA YA MWILI, TAMAA YA MACHO NA KISHA KIBURI CHA UZIMA. Tamaa ina nguvu ya kuvuta pamoja na kudanganya, naam inamuingiza mtu kwenye jaribu. Hii ina maana tamaa ni mlango, naam mlango huu unapaswa kufungwa mapema usikupoteze. Hebu tujifunze kutokana na anguko la mfalme Daudi na mke wa Bathssheba (Samweli 11:1-2). Tunaona anguko la Daudi lilisaabishwa na kumpa Ibilisi nafasi kwa kutokwenda vitani. Mkristo akipoa katika kuvipiga vita vya kiroho inakuwa rahisi kwake kuanguka dhambini (Yakobo 1:14-15), naam kumbuka kwamba siku zote tamaa inalenga kumfurahisha mtu binafsi (self-pleasing) bila kujali matokeo yake.
Hivyo katika nyakati tulizonazo sasa suala la kuipenda dunia ni lazima litafutiwe ufumbuzi wa kudumu miongoni mwa vijana wetu. Ujumbe huu mfupi unalenga kueleza kwa namna gani kuipenda dunia kumekuwa tanzi kwa vijana na nini vijana wafanye ili kuikabili na kuishinda changamoto husika.
Pia katika waraka 2Timotheo 2:15 Mtume Paulo anaendelea kumwambia kijana Timotheo ‘Jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa na Mungu, mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, ukitumia kwa halali neno la kweli’.
Pengine kila mmoja wetu atafakari maisha yake kwa kuhusianisha na maelekezo ya Paulo kwa Timotheo. Naomba jiulize na kujijibu kwa uaminifu kwamba mosi, je, ujana wako wako unaheshimika au unadharauliwa? Pili, je, kwa waamini wenzako umekuwa kielelezo cha kweli kwa habari ya imani, upendo, usafi, usemi na mwenendo au la?
Binafsi nimekuwa nikijiuliza ni kwa namna gani kijana atahakikisha kwamba (a) Ujana wake haudharauliwi (b) Anakuwa kielelezo kwa waamini wenzake (c) Anathibitisha kwamba kweli amekubaliwa na Mungu. Naam katika kusoma na kutafakari neno la Mungu nimejifunza kwamba zifuatazo ni njia ambazo zitatusaidia sisi vijana wa leo kuifikia kweli hii ya neno la Mungu.
• Kijana adumu katika kuomba na kusoma (kutafakari + kulitenda) neno la Mungu
Katika Zaburi 119:9 & 11 Biblia inasema ‘Jinsi gani kijana aisafishe njia yake? Kwa kutii AKILIFUATA neno lako’. Pia kwenye ule mstari wa 11 inasema ‘moyoni mwangu nimeliweka neno lako, NISIJE NIKAKUTENDA DHAMBI’.
Naam katika Mathayo 26:41 imeandikwa ‘Kesheni, mwombe, MSIJE mkaingia majaribuni; roho I radhi, lakini mwili ni dhaifu’. Yohana 17:17 inasema ‘uwatakase kwa ile kweli ;neno lako ndiyo kweli. Mambo haya mawili yanapaswa kwenda kwa pamoja nakijana akidumu katika kuomba na kusoma neno la Mungu ushindi ni lazima.
• Kijana asimpe Ibilisi nafasi.
Kijana anapaswa kujiuepusha na mazingira yenye kumfanya aiepende na kuifuatisha namna ya dunia hii. Katika kitabu cha 1Wakorinto 6:12 imeandikwa ‘Vitu vyote ni halali kwangu, lakini si vyote VIFAAVYO; vitu vyote ni halali kwangu, lakini mimi sitatiwa chini ya UWEZO wa kitu chochote’. Ni vizuri ukahakikisha kwamba ufahamu wako hautawaliwi na mambo yasiyo ya msingi (non-essentials of life) – Je ufahamu wako umetawaliwa ni nini?
Hii ndiyo sababu iliyomfanya Paulo awaambie Waefeso ‘Wala msimpe Ibilisi nafasi’ (Waefeso 4:27) na pia awaambie Warumi “Bali mvaeni Bwana Yesu Kristo, wala msiuangalie mwili hata kuwasha tamaa zake’. Toleo la KJV linasema ‘But put ye on the Lord Jesus Christ, and MAKE NOT PROVISION for the flesh, to fulfill the lusts thereof’. Na toleo la ESV linasema ‘But put on the Lord Jesus Christ, AND MAKE NO PROVISION FOR THE FLESH, TO GRATIFY ITS DESIRES’ (Warumi 13:14). Je hivi leo ni kwa namna gani vijana wanaungalia mwili na kumpa Ibilisi nafasi? – Mitandao ya kijamii, kuangalia na kusoma vitu vichafu, hasira, mawazo, mazingira.
• Kijana azikimbie tamaa za ujanani
Katika 2Timotheo 2:22 imeandikwa ‘LAKINI ZIKIMBIE TAMAA ZA UJANANI; ukafuate haki, na imani, na upendo, na amani, pamoja na wale wamwitao Bwana kwa moyo safi’. Kijana anawezaje kuzikimbia tama za ujanani? Hebu tuangalie mfano wa Yusufu. Ushindi wa Yusufu dhidi ya mke wa Uria (Mwanzo 39:2-9). Hii ni habari ya kijana Yusufu ambaye alikuwa msimamizi mkuu wa mali za Potifa.
Pamoja na ushawishi aliokutana nao Yusufu alijibu kwamba ‘Nifanyeje ubaya huu mkubwa nikamkose Mungu?’ Mwanzo 39:12 inasema ‘huyo mwanamke akamshika nguo zake, akisema, Lala nami. Yusufu akaiacha nguo yake mkononi mwake akakimbia akatoka nje. Ili kuzikimbia tamaa za ujanani kijana anapswa (a) ajiepushe na mazingira/marafiki wabaya (Mithali 1:10 & 1Wakorinto 15:33) (b) Ajitenge na uovu (Mithali 16:17, Zaburi 1:1).
Ni muhimu ukakumbuka kwamba hukupewa mwili kwa ajili ya zinaa maana miili yenu ni ni viungo vya Kristo na tena hekalu la Roho Mtakatifu (1 Wakorinto 6:15 & 19), tena yeye aliyeungwa na Bwana ni roho moja naye (1 Wakorinto 6:17) maana tena imeandikwa ‘Lakini mwili si kwa zinaa, bali ni kwa Bwana, naye Bwana ni kwa mwili’ (1Wakorinto 6:13b). Tena imeandikwa ‘Lakini uasherati USITAJWE kwenu kamwe, wala uchafu wowote wa kutamani, kama iwastahilivyo watakatifu’ (Waefeso 5:3).
• Kijana ajifunze kuenenda kwa roho na si kwa mwili
Katika wagalatia 5:16 imeandikwa ‘Basi nasema ENENDENI KWA ROHO, wala HAMTATIMIZA kamwe TAMAA ZA MWILI. Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili; kwa maana hizi zimepingana, hata hamwezi kufanya mnayoyataka’.
Je kuenenda kwa Roho ndio kukoje?
Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, ATAWAONGOZA awatie kwenye kweli yote (Yohana 16:13) na pia imeandikwa ‘kwa kuwa wote WANAOONGOZWA na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu’ (Warumi 8:14). Kuenenda kwa Roho ina maana ya kuishi kwa kufuata utaratibu/uongozi wa Roho Mtakatifu kwenye maisha yako (Warumi 8:2).
Naam kadri unavyokuwa mtiifu kufuata utaratibu wake ndivyo unavyokuwa mbali na sheria ya dhambi na mauti ambayo ni mwili. Kumbuka imeandikwa ‘kwa maana wale waufuatao mwili huyafikiri mambo ya mwili; bali wale waiufuatao roho huyafikiri mambo ya roho. Kwa kuwa nia mwili ni mauti bali nia ya roho ni uzima na amani (Warumi 8:5-6) na pia Wafilipi 4:8.
Naam imeandikwa ‘Kila mmoja wenu ajue KUUWEZA MWILI wake katika utakatifu na heshima; si katika hali ya tamaa mbaya, kama mataifa wasiomjua Mungu. Maana Mungu HAKUTUITIA UCHAFU, bali tuwe katika utakaso’ (1Thesalonike 4:4-5, 7). Ni jambo la ajabu sana kwamba kwamba tumepewa fursa ya kuiweza miili yetu. Ndio tunapaswa kuuweza mwili kwa maana ya kuudhibiti kwa kuuongoza na kuufanya ufuate nia ya roho.
Kijana mwenzangu kama umechagua kumpa Yesu maisha yako kwa njia ya wokovu, nakusihi na kukushauri zingatia haya ili kuwa na maisha yenye kielelezo na ushuhuda mzuri maana imeandikwa ‘Kwa maana wale waliokwisha kuyakimbia machafu ya dunia kwa kumjua Bwana na Mwokozi Yesu Kristo, kama wakinaswa tena na kushindwa, hali yao ya mwisho imekuwa mbaya kuliko ile ya kwanza. Maana ingekuwa heri kwao kama wasingaliijua njia ya haki, kuliko kuijua, kisha kuiacha ile amri takatifu waliyopewa’ (2Petro 2:20-21).
AMENI