PENUEL GLORIOUS MINISTRY OF TANZANIA

PGMT

ASKOFU WA KANISA LA PENUELI MAKAO MAKUU MPANDA KATAVI

Monday, October 13, 2025

SOMO:NEEMA YA MUNGU - 2

Jambo la Pili : Neema moja inaweza kukusaidia kuomba na kupata Neema zingine. Angalia kwenye Biblia; Kutoka 33:13 …Basi, sasa nakuomba, ikiwa nimepata neema mbele zako, unionyeshe njia zako, nipate kukujua, ili nipate neema mbele zako; ukakumbuke ya kuwa taifa hilo ndilo watu wako. Musa alipokuwa anafanya maombi alisema kuwa, kama amepata Neema mbele za Mungu, 'apate neema mbele zake'. Ukisoma hiyo sentensi ina neno 'neema' mara mbili; yaani kuna 'neema' mbili tofauti zinazungumziwa kwenye mstari mmoja. Neema ya kwanza anayoitaja ni Neema ambayo inamsaidia kwenye kuomba vitu vingine. Ni msingi wa maombi yake, kwa sababu haanzi kuomba kwanza mpaka ameuliza kama ana Neema za kusongea mbele za Mungu ili kufanya maombi ya vitu vingine. Neema ya pili inayotajwa kwenye mstari ni ombi. Anaomba apate neema. Na ili apate hii neema ya pili lazima awe na neema ya kwanza aliyoitaja. Asipopata neema ya kwanza maana yake na Neema ya pili ataikosa. Neema ya pili ni ombi la yeye kutaka Mungu awe pamoja naye ili kuwaongoza wana wa Israel kuelekea Kanaani. Kwa hiyo neema moja inaweza kukusaidia kuomba neema nyingine. Si wengi sana wanaojua kuwa neema zipo nyingi. Kuna neema nyingi sana lakini ufunguo wa neema zote tunazopokea ni Yesu Kristo, maana ndiye aliyekuja na Neema na kweli (Yoh 1:17). Kwahiyo Neema ya kwanza inayoweza kukusaidia kuombea neema zingine ni Neema ya kuwa na Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wa maisha yako. Ndani yake yeye (Yesu) ndimo tunachota kila aina ya Neema, na ndio maana tunasema tupo kwenye kipindi cha neema na siyo kipindi cha sheria kama ilivyokuwa kwenye Agano la kale. Msingi wa Agano jipya ni neema. Yohana 1:16 …Kwa kuwa katika utimilifu wake {Yesu} sisi sote tulipokea, na neema juu ya neema. Biblia ipo wazi, inasema katika utimilifu wake Yesu Kristo (alitimilika msalabani) tulipokea na neema juu ya neema. Kupitia msalaba wa Yesu kristo siyo tu kwamba tunapata neema, bali tunapata na neema juu ya neema . Maana yake kupitia msalaba unaweza ukapata neema nyingi tu. Neema ya kumwamini Yesu Kristo na kuamini alichokifanya msalabani ni mlango wa wewe kupokea neema zingine nyingi. Nachotaka uone pia ni kwamba neema siyo moja, zipo neema nyingi sana ambazo ziliachiliwa msalabani ni kazi yetu sisi kuzichukua. Ndiyo maana kwenye Biblia anasema 'tulipokea na neema juu ya neema'. Anatumia neno 'tulipokea' na siyo tutapokea. Anatumia wakati uliopita na siyo uliopo. Maana yake neema zilishakuja kupitia msalaba, siyo zitakuja, bali zilikuja! Ni swala la sisi tu kuzichukua msalabani tu. 2 Wakorintho 9:8 ….Na Mungu aweza kuwajaza kila neema kwa wingi, ili ninyi, mkiwa na riziki za kila namna siku zote, mpate kuzidi sana katika kila tendo jema; Matendo ya Mitume 4:33 …Na mitume wakatoa ushuhuda wa kufufuka kwake Yesu kwa nguvu nyingi, na neema nyingi ikawa juu yao wote Ukisoma kwenye hiyo mistari utagundua kitu kwamba Neema zipo nyingi na wala haipo moja. Tupo kwenye kipindi cha Neema kwa sababu tupo kwenye kipindi cha kupitia utimilifu wa Yesu msalabani tulipokea Neema nyingi. Wakorintho inatwambia kwamba Mungu aweza kuwajaza kila Neema kwa wingi, Neno 'kila' linaonyesha kwamba zipo nyingi lakini Mungu anaweza kukujaza zote. Kama Mungu anaweza kutupa kila Neema basi na tupige magoti kwake atupe Neema / za kutosha. Kuna neema ya kumjua Mungu ;kuna neema ya kumtumikia Mungu ; kuna Neema ya kushiriki ibada, n.k Omba Mungu akupe Neema nyingi ili uwe kwenye kipindi cha neema kweli kweli, kuliko unatamba kwa watu kwamba upo kwenye kipindi cha Neema kumbe hata nini maana ya Neema hujui. Jambo la 3: Neema yako inaweza kuwabeba na watu wengine. Neema ipo kwa ajili ya kutufanya tuishi ndani ya kusudi la Mungu. Na kusudi la Mungu ni kwa ajili ya watu wa Mungu. Kwa hiyo unaweza ukapewa Neema wewe ila ikawasaidia na wengine! Angalia kwenye Biblia; 1 Petro 4:10 …kila mmoja kwa kadiri alivyoipokea karama, itumieni kwa kuhudumiana; kama mawakili wema wa neema mbalimbali za Mungu. Biblia inatuonyesha kuwa kama mawakili wa Neema inatubidi tuwe tunahudumiana kwa kadiri ya karama ya kila mmoja wetu. Ni kama anataka kutwambia kwamba Neema uliyopata iliyokupa hiyo Karama itumie kwa ajili ya kuwahudumia wengine , Maana ukirudi kwenye jambo la kwanza nilikwambia kuwa NEEMA ya Mungu ndiyo inaonyesha kusudi/ huduma/ Karama ya Mungu kwenye maisha yako. Ukipokea neema ya Mungu itumie kuhudumia watu. Kutoka 33:16 ..Kwa maana itajulikanaje kuwa nimepata neema mbele zako, mimi na watu wako? Siyo kwa sababu unakwenda pamoja nasi, hata mimi na watu wako tutengwe na watu wote walio juu ya uso wa nchi? Musa aliomba Neema yeye pekee yake kwenye mstari wa 13. Kwenye mstari wa 16 anataka kujua kama Neema aliyoomba itawasaidia na wenzake? Maana yake Musa alijua kabisa kwamba akipata Neema yeye itawasaidia na watu wengine pia. Mwanzo 6:8 …Lakini Nuhu akapata neema machoni pa BWANA. Wasomaji wa Biblia wanajua kwamba Neema aliyoipokea Nuhu haikumsaidia yeye pekee yake, bali iliokoa uhai wa mbegu ya viumbe hai duniani na uhai wa watu nane, yaani Nuhu, hamu, yafethi na Shemu pamoja na wake zao; lakini hao saba hawakupata Neema isipokuwa Nuhu pekee yake, na kwa sababu hiyo wengine wote saba waliokolewa kwa faida ya Neema iliyokuwa kwa Nuhu. Ukipata Neema tambua kuwa ni kwa ajili ya watu pia. Mungu atusaidie. Jambo la 4: Unaweza ukawa na Neema ya Mungu lakini isijae. Neema ya Mungu ina kipimo chake, inaweza kujaa au kutokujaa. Sasa unaweza ukawa una Neema ya Mungu lakini ikawa haijajaa katika kiwango kinachotakiwa. Ngoja tuangalie kwenye Biblia alafu uone kitu huko. Matendo ya Mitume 6:8 ..Na Stefano, akijaa neema na uwezo, alikuwa akifanya maajabu na ishara kubwa katika watu. Biblia inamtaja stefano kama mtu aliyejaa Neema. Kama Biblia imemtaja stefano kuwa alijaa Neema maana yake walikuwepo watu wengine ambao hawakujaa Neema, japokuwa walikuwa nayo. Je wewe umejaa Neema ya Mungu? Imani yako katika kristo ndiyo itaamua neema iweje ndani yako. Waebrania 12:15 …mkiangalia sana mtu asiipungukie neema ya Mungu; shina la uchungu lisije likachipuka na kuwasumbua, na watu wengi wakatiwa unajisi kwa hilo. Waebrania inatwambia kuwa mtu asiipungukie neema ya Mungu. Na anatoa ni tahadhari maana anaanza kwa kusema, mkiangalia sana, mtu asiipungukie neema ya Mungu; ni tahadhari hii. Kwa hiyo kama mtu hataangalia sana [ kama hatachukua tahadhari ] anaweza kujikuta ameipungukia neema ya Mungu kwa kujua au kwa kutokujua. Imani yako thabiti juu ya Yesu Kristo na kile alichokifanya msalabani basi ndiyo itakufanya uendelee kuwa na neema ya Mungu yote. Ukiugeuzia mgongo msalaba na Neema ya Mungu inaanza kupungua kwako. Tunapokea Neema kwa njia ya msalaba kupitia Yesu Kristo. Msisitizo upo kwenye kutambua kuwa inawezekana unaishi ukiwa na Neema ya Mungu lakini ikiwa ni ndogo sana; chukua tahadhari. INAENDELEA SEHEMU YA TATU

Saturday, October 11, 2025

SOMO : NEEMA YA MUNGU -1

SOMO : NEEMA YA MUNGU KITABU CHA SOMO: Warumi 12:6 …Basi kwa kuwa tuna karama zilizo mbalimbali, kwa kadiri ya neema mliyopewa; ikiwa unabii, tutoe unabii kwa kadiri ya imani; Na Askofu Mkuu Dr. Burton Saulo Yuda. Maana ya Neema ya Mungu ni kipawa kutoka kwa Mungu au ni upendeleo unaokuja toka kwa Mungu kupitia Yesu kristo kwenye maisha yetu. Neema ya Mungu ni kitendo cha kustahili mahali ambapo hatukustahili. Ni kufaa eneo au mahali ambapo hatukufaa tuwe. Ni kipawa toka kwa Mungu mwenyewe kutupa kitu au vitu ambavyo hatukustahili. Mtu yeyote asijisifu kwa chochote kile. Vipo vitu kadha vya msingi kuvijua kuhusu Neema ya Mungu. Kwenye somo hili tutajifunza mambo saba muhimu ya kuhusu Neema ya Mungu. Jambo la kwanza : Neema inabeba kusudi la Mungu kwenye maisha yetu. Si wengi sana wanaojua kuwa unaweza ukaombewa au ukaomba kwa Mungu na ukapata Neema ya Mungu ambayo ulikuwa huna. Tuliangalia huko juu kuwa Mungu anaweza kutupa 'kila' Neema. 2 Wakorintho 9:8 Na Mungu aweza kuwajaza kila neema kwa wingi, ili ninyi, mkiwa na riziki za kila namna siku zote, mpate kuzidi sana katika kila tendo jema. Huu mstari unaonyesha wazi kwamba Mungu 'anaweza' kutupa kila Neema. Na kama Mungu anaweza kutupa 'kila' Neema maana yake kumbe tuna uwezo wa kusogea msalabani pake na tukapata Neema tunayoihitaji. Kumbuka Neema zimekuja kupitia utimilifu wa Yesu pale msalabani. Kwa hiyo kama tukitaka kupata Neema ya Mungu, na tuusogelee msalaba wa Yesu kwa imani ili tupate Neema zilizoachiliwa hapo msalabani. Kama unahisi hakuna Neema juu ya maisha yako muombe Mungu kwa imani nayo utaipata (kama ni kwa mapenzi Si watu wengi wanaofahamu kuwa kusudi la Mungu kwenye maisha yao limebebwa kwenye kitu kinachoitwa NEEMA YA MUNGU. Ngoja tuangalie maandiko uone; Warumi 12:6 Basi kwa kuwa tuna karama zilizo mbalimbali, kwa kadiri ya neema mliyopewa; ikiwa unabii, tutoe unabii kwa kadiri ya Imani. Paulo a.navyowaambia warumi kwamba tuna Karama mbalimbali lakini kwa 'kadri ya Neema' tuliyopewa. Ile Neno 'kwa kadri' linaonyesha kipimo. Maana yake kipimo cha Karama tulizonazo ni Neema ya Mungu. Kama Neema ya Mungu ni kubwa kwako, hata Karama itakuwa kubwa pia. Kama Neema ya Mungu ni ndogo hivyo hivyo pia na Karama itakuwa ndogo; maana Karama ni kwa kadri ya Neema tuliyopewa. Tunajua kuwa Karama tulizopewa zipo kwenye kusudi la Mungu kutuumba na kutuweka duniani. Kwa hiyo kama Neema ya Mungu ndiyo kipimo cha Karama basi Neema ya Mungu inabeba kusudi la Mungu kwenye maisha yetu. Neema kubwa inabeba kusudi kubwa, Neema ndogo inabeba kusudi dogo. Lile Neno 'kwa kadri' linaonyesha kuwa viwango vya Neema vinatofautiana. Waefeso 4:7 Lakini kila mmoja wetu alipewa neema kwa kadiri ya kipimo cha kipawa chake Kristo. Angalia hapo kwenye waefeso jinsi Biblia inavyosema. Biblia inasema kwamba kila mmoja alipewa neema kwa kadiri ya kipimo cha kipawa chake kristo. Maana yake kila mmoja amepewa Neema kwa kipimo ambacho Yesu Mwenyewe alipenda kugawa au kumpa. Kwahiyo kuna watu wana Neema kubwa na kuna watu wana Neema kidogo, lakini si kwa sababu ya matendo bali ni kwa sababu ya kipawa chake Kristo. Nataka uone hiki kitu, Neema zinatofautiana. Na sio wengi wanaojua kuwa Neema zinatofautiana. na watu kutokujua kuwa Neema zinatofautiana basi kuna muda wale wenye Neema kubwa wanaona wenye Neema ndogo kama wavivu hivi; na wale wenye neema ndogo wanaona kama wao hawafai katika kazi ya Mungu; lakini haipo namna hiyo. Utofauti wa Neema unakuja kutokana na utofauti wa kusudi la mtu na Karama ya Mtu. Neema zingefanana maana yake wote tungekuwa na kusudi moja! Sasa kwa sababu makusudi ya Mungu kwa mwanadamu ni tofauti tofauti basi hata Neema tunapewa tofauti tofauti na kwa kipimo tofauti tofauti. Neema iliyo kwangu mimi mwalimu haiwezi kufanana na Neema anayopewa mwinjilisti au mchungaji. Ndivyo hata warumi 12:6 imetuambia. Vipo vipengele kadha nataka uvione kwenye hili jambo la kwanza. a. Kazi ya Neema ni kukupitisha kwenye kusudi la Mungu. Ili kujifunza hiki kipengele natamani tutazame mifano kadhaa. Mfano 1. Nuhu. Mwanzo 6:8 .. Lakini Nuhu akapata neema machoni pa BWANA. Wasomaji wa Biblia wanajua kuwa mwanadamu wa kwanza kupata Neema kwenye Biblia ni Nuhu. Kwa wale ambao hawajapata Neema ya kusoma Biblia, Nuhu ni yule jamaa ambaye alijenga Safina wakati wa gharika, bila shaka umewahi kusikia habari zake. Nachotaka uone kwa huyu ndugu Nuhu ni kwamba, popote utakapoona pana Neema ya Mungu basi ujue kuna kusudi la Mungu. Ukipewa Neema tu inakupitisha kwenye kusudi la Mungu. Ngoja tuseme hivi, Mungu alivyoona maasi kwa mwanadamu yameongezeka alipanga kutoa adhabu kwa kutumia mvua kubwa iletayo mafuriko makubwa (gharika) lakini Mungu hakutaka kuharibu kusudi lake na viumbe hai kuijaza Dunia. Kw hiyo Mungu akawa anamtafuta mtu atakaye mbebesha hilo kusudi ili atunze mbegu za viumbe hai. Biblia inasema Nuhu akapata 'Neema'. Kumbuka tulikotokea, ukiona Neema ya Mungu mahali ujue kuna kusudi la Mungu. Kwa hiyo Neema aliyoipata Nuhu ilikuwa kwa ajili ya kusudi la kutunza mbegu za viumbe hai duniani ambalo Mungu alimpa huyu ndugu Nuhu. Neema ya Mungu inakupa kusudi la Mungu kwenye maisha yako. Je unaifahamu Neema ya Mungu kwako, na ina kusudi gani? Mfano 2. Mariamu. Luka 1:28 Akaingia nyumbani kwake akasema, Salamu, uliyepewa neema, Bwana yu pamoja nawe. Mariamu alipewa salamu na malaika Gabrieli, salamu ilitaja Neema ya Mungu. Maana yake Mariamu alikuwa amepewa Neema ya Mungu, na kwa sababu neema ya Mungu inabeba kusudi fulani bila shaka hii Neema ya Mungu haikuwa bure pia, ilibeba kusudi ndani yake! Je unajua ni kusudi gani hilo? Luka 1:31…Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu. Kusudi lililobembwa kwenye Neema aliyopewa Mariamu ilikuwa ni kutimiza kusudi la Mungu la kumleta Yesu Kristo duniani ili aje aichukue dhambi ya ulimwengu! Ukipewa Neema na haujaielewa muulize aliyekupa Neema kama Mariamu alivyofanya. Aliuliza hii salamu ni ya namna gani? Alafu akapewa jibu. Mfano 3. Esta. Esta 2:17 Mfalme akampenda Esta kuliko wanawake wote, naye akapata neema na kibali machoni pake kuliko mabikira wote; basi akamtia taji ya kifalme kichwani pake, akamfanya awe malkia badala ya Vashti. Esta alipata Neema machoni pa mfalme Ahausuero baada ya aliyekuwa malikia (Vashti) kuonyesha dharau kwa mfalme. Esta akapata neema kwa mfalme ya kuweza kuchukua nafasi ya malkia Vashti. Sasa nataka utazame katika jicho la Mungu, yaani Mungu anamwonaje Esta? Mungu alimbebesha kusudi kubwa sana Esta kwa ajili ya wayahudi. Mungu alikuwa anamwandaa Esta kwa kuja kuwatoa katika hatari ya kuuawa ambayo Hamani angeitangaza siku chache mbele. Kwa hiyo nataka ujifunze hiki, aliyesababisha mfalme Ahausuero ampe Neema Esta ni Mungu mwenyewe. Yaani hivi, Mungu alimpa neema Esta ili apate neema mbele ya mfalme ili kusudi la Mungu litimie. Kabla mfalme hajampa neema Esta, Mungu alikuwa tayari amekwisha kumpa Esta Neema ili kuwalinda wayahudi wasiuawe na Hamani. Kuna muda tunapata neema (upendeleo) kwenye mashule, maofisini au kazini sio kwa sababu maboss zetu wametupenda tu bali ni kwa sababu Mungu ametupa Neema yake kwa ajili ya kusudi analotaka litimie kwenye hiyo shule, au chuo, au ofisi n.k Usipojifunza kufanya kazi na Mungu popote ulipo utajikuta unapata Neema (upendeleo) mahali ulipo alafu ukabaki unashangaa tu, ukawa mzigo kwa Mungu badala ya kuwa msaada kwa Mungu kutimiza kusudi lake! Mfano 4. Paulo. Wagalatia 1:15 Lakini Mungu, aliyenitenga tangu tumboni mwa mama yangu, akaniita kwa neema yake, Paulo anasema Mungu alimtenga tangu tumboni mwa mama yake, akamwita kwa 'neema' yake. Tunajua kuwa ni kweli Mungu alimtenga Paulo kwa ajili ya kazi yake. Kwa hiyo alimwita kwa NEEMA yake , Ni kama anataka kutwambia kwamba Neema ya Mungu ndiyo iliyobeba kusudi la yeye kutengwa toka tumboni mwa mama yake. Na neema hii ya Paulo ilikuwa kwa ajili ya kusambaza injili kwa mataifa (kwa watu wasio wayahudi) Nimekupa hii mifano ili uone na ujue kuwa Neema ya Mungu haiji bure, inakuja na kusudi la Mungu. b . Kiwango cha kuishi ndani ya kusudi la Mungu kunategemea kiwango cha Neema. Neema ya Mungu ina kipimo tofauti tofauti, inaweza kuwa kubwa au ndogo. Sasa, kiwango cha wewe kuishi ndani ya kusudi la Mungu ,Kunategemea sana kiwango au kiasi cha Neema uliyo nayo! Ukiangalia maisha ya Paulo na maisha ya petro au maisha ya Yohana yalitofautiana. Kitu kilichotengeneza utofauti wao ni kiwango na aina ya Neema waliyokuwa wamepewa. Ngoja tusome kwenye Biblia uone kitu; 1 Wakorintho 15:10 ..Lakini kwa neema ya Mungu nimekuwa hivi nilivyo; na neema yake iliyo kwangu ilikuwa si bure, bali nalizidi sana kufanya kazi kupita wao wote; wala si mimi, bali ni neema ya Mungu pamoja nami. Ukisoma kwenye huu mstari unaona vitu kadha ndani yake. i) Maisha ya Paulo yalitegemea Neema aliyopewa na Mungu. Ukisoma huu mstari unaona Paulo anawaambia wakorintho kuwa "nimekuwa hivi nilivyo kwa Neema ya Mungu". Maana yake Neema ya Mungu ndiyo ilimfanya Paulo awe Paulo ambaye tunamfahamu. Huenda angeendelea kuishi nje na neema ya Mungu Paulo angeendelea kuwa muuaji na mpinzani namba moja wa injili. Kwa hiyo kilichomfanya Paulo abadilike toka kuwa mpinzani wa injili mpaka kuwa mhubiri wa injili ni Neema ya Mungu. Alafu mbele ya huo mstari anasema "nalizidi sana kufanya kazi kupita wao wote (mitume 12); wala si mimi, bali ni neema ya Mungu pamoja nami". Paulo anachotaka tuone ni kwamba, ile huduma aliyoifanya, kazi yote aliyoifanya na jinsi alivyofanya kazi kuzidi hata wale mitume 12 waliokuwa na Yesu kila mahali; kuwa ni Neema ya Mungu. Si kwa elimu, si kwa akili, si kwa mali wala ujuzi bali ni kwa neema ya Mungu. Maana yake bila Neema ya Mungu asingekuwa jinsi alivyo. Swali nililojiuliza ni kitu gani kilitofautisha kazi aliyoifanya Paulo na mitume wengine? Biblia inatoa jibu kuwa ni Neema ya Mungu. Kwahiyo hata wewe maisha yako jinsi yalivyo ni kwa Neema ya Mungu. Mimi mwenyewe jinsi nilivyo ni kwa Neema ya Mungu. Ukielewa hivi itakusaidia sana. Nimeona watu wengi sana wakiwa wanaiga huduma na Karama za watu. Lakini hawajui kama Neema iliyo juu ya wale watu anaowaiga na Neema iliyo juu yake ni tofauti! Sasa ukitaka uharibu kazi endelea kung'ang'ania huduma ya mtu wakati mna neema tofauti kabisa. Hata hivyo unapata wapi ujasiri wa kumuiga mtu au kujifananisha na mtu? Watu wengi sana ambao somo la Neema ya Mungu limewapita pembeni (hasa vijana) huwa wanafanya huduma mda mwingine kwa kushindana. Au wanafanya huduma kwa kuiga, au kwa kujifananisha na fulani. This is foolishness! A spiritual ignorance! Neema ya Mungu ndio itakuelezea wewe huduma yako ipoje na watu gani utawahudumia na mipaka ya huduma yako ni ipi. Kazi ya Mungu hatushindani, hatugombaniani, wala hatuigi; tunafanya kwa NEEMA ya Mungu. ii) Neema ya Mungu inaweza kuwa ya bure. Kutoka kwenye mstari wa 1 kor 15: 10 tunaona kitu cha pili pale, kuwa; Neema ya Mungu inaweza kuwa ya bure. Paulo anasema: "na Neema yake iliyo kwangu ilikuwa si bure!" Kama Paulo alisema hivi maana yake kuna muda na kuna watu Neema ya Mungu ni bure kwao yaani haifanyi kazi. Unaijua hatari ya kuwa na Neema ya Mungu alafu ikawa ya bure? Ukiona unaishi maisha ambayo nafsi yako tu inakushuhudia kwamba kuna jambo unapaswa kulifanya kiroho au kimwili na umelinyamazia ujue Neema ya Mungu ni bure kwako. Neema ya Mungu kuwa bure kwako ni kuishi chini ya viwango vya kusudi la Mungu kwenye maisha yako. Kuna mtu alinitafuta akaniambia mtumishi ninaona deni kubwa sana moyoni mwangu. Nina huduma kubwa sana ambayo Mungu ananishuhudia ndani yangu lakini maisha ninayoishi ni tofauti kabisa na huduma yangu. Kama wewe ni sawa na huyu mtu basi ni kwamba Neema ya Mungu iliyo ndani yako haifanyi kazi sawa sawa. Inabidi uingie kwenye maombi ya toba na maombi ya kukusaidia kuanza kufanya kazi ya Mungu. Mungu ni mwaminifu, atakujibu. Au unaweza kwenda na sadaka madhabahuni na ukaombewa, maana neema ya Mungu unaweza ukaombewa na ukaipata. Kikubwa chunga sana, Neema ya Mungu isiwe bure kwenye maisha yako, kwa sababu ikiwa ni bure maana yake unakwamisha kazi ya Mungu. Na mti ambao hauzai hukatwaa na kutupwa mbali ili inayozaa ipate nafasi na hewa kubwa zaidi ili izae sana! Je unataka kukatwa? Waefeso 3:7 …Injili hiyo ambayo nalifanywa mhudumu wake, kwa kadiri ya kipawa cha neema ya Mungu niliyopewa kwa kadiri ya utendaji wa uweza wake. Paulo alifanywa kuwa mhudumu wa injili ‘kwa kadri ya kipawa cha Neema ya Mungu’. Kwa hiyo huduma na namna unavyotakiwa kufanya vinatokana na Neema ya Mungu. Siku moja kuna mtumishi aliniita na kuniambia jambo. Akaniambia kuwa mimi nina huduma kubwa sana na akasema anashangaa kuona naongea na kila mtu, yaani waliookoka, waislamu na wapagani vizuri kabisa, na akaniambia kuwa yeye hawezi kutengeneza urafiki na watu wa dunia wakati yeye ni mhudumu (alikuwa mwinjilisti). Nikamjibu kivyepesi sana nikasema, sisi wote ni watumishi wa Mungu, lakini utofauti wa huduma na aina ya maisha tunayoishi yanatokana na kiwango cha Neema ya Mungu ambacho hakiwezi kufanana, na kama Neema hazifanani hata maisha yetu hayawezi kufanana. Nikamwambia jinsi maisha nayoishi ya kuwa na marafiki bila kujali dini jinsi yalivyonisaidia kukutana na watu wenye shida mbalimbali za kiroho na nikaweza kuwasaidia tofauti na kama ningekuwa nabagua. Nikamwambia kuwa, mimi siwezi kuishi kama yeye na yeye hawezi kuishi kama mimi kwa sababu Neema zinatofautiana na kila penye neema pana kusudi la Mungu; kama ambavyo tumejifunza huko juu. Sasa sikuambii na wewe uwe na marafiki bila kujali hali zao za kiroho, Wakikupoteza shauri yako Maana neema hiyo niliyopewa huenda wewe huna. Ndio maana kwenye mazungumzo yetu sikumhukumu wala yeye hakunihukumu kwa sababu ukinihukumu ninavyoishi ni umeihuku Neema ya Mungu inayonifanya niishi hivyo. Muda mwingine watumishi wa Mungu wanatengeneza tumigogoro kwa sababu ya vitu vinavyotengenezwa na Neema ya Mungu. Ila sina maana kila ugomvi unatokea hapo, no! Nataka tu uone na ujifunze jambo. Jifunze hili somo la Neema ya Mungu itakusaidia sana. Mungu akusaidie uelewe zaidi ya hapa ili uweze kulifanyia kazi vizuri. Limekuja kwako kwa wakati wa BWANA kabisa. 2 Wakorintho 6:1 ..Nasi tukitenda kazi pamoja naye twawasihi msiipokee neema ya Mungu bure. Msisitizo upo kwenye 'msipokee neema ya Mungu bure'. Hapa nataka kukupa msisitizo kwenye lile jambo la pili kwenye kile kitabu cha 1 kor 15:10 kuwa NEEMA ya Mungu inaweza ikawa bure kwako. Kama Paulo anavyowasihi wakorintho na mimi pia nawasihi leo watanzania wenzangu na mlio nje ya nchi katika jina la Yesu kristo, msiipokee Neema ya Mungu bure. Ni wachache wamepata neema toka kwa Mungu, sasa na sisi wachache tuliopewa Neema ya Mungu tukiifanya iwe bure tunaharibu kazi ya Mungu aliyotupea Neema katika kusudi lake duniani. c. Neema ya Mungu inakufundisha namna ya kufanya na namna ya kuishi. Kutoka 33:13….Basi, sasa nakuomba, ikiwa nimepata neema mbele zako, unionyeshe njia zako, nipate kukujua, ili nipate neema mbele zako; ukakumbuke ya kuwa taifa hilo ndilo watu wako. Musa aliomba kwamba kama amepata Neema mbele za Mungu basi Mungu amwonyeshe njia. Maana yake Musa alijua kuwa bila Neema ya Mungu asingeweza kupata njia! Ndio maana haanzi kuomba kuona njia bali anatanguliza kwanza kuomba NEEMA YA MUNGU, akiwa anajua kuwa Neema ya Mungu ikija itakuja na njia ya Mungu ndani yake. Musa baada ya maombi ya muda mrefu, alipata NEEMA mbele za Mungu na Mungu akaanza kumwonyesha njia ya kuwaongoza wana wa Israel kuelekea Kanaani. Kumbuka kuwa Musa aliingia kwenye haya maombi baada ya Mungu kughairi kuwaongoza na akataka atume malaika ndiye awaongoze kwenda Kanaani ndipo Musa alipoomba Neema ya Mungu. Sasa nataka uelewe kuwa Neema ya Mungu ndiyo inaweza kukusaidia kukuonyesha njia ya wapi upite kwenye kusudi Mungu aliloliandaa maishani mwako. Nimekuambia kuwa palipo na Neema ya Mungu pana kusudi la Mungu na kwa hiyo Neema haiishii tu kukupa kusudi bali pia inakupa njia ya kulifikia kusudi la Mungu kwenye maisha yako! Wengine wanatangatanga hawajui waanzie wapi kutimiza kusudi la Mungu, lakini jibu ni jepesi sana, ni kutafuta na kuomba NEEMA ya Mungu kama Musa alivyofanya. Neema ya Mungu ni ‘set’ kamili inayobeba vitu vyote unavyohitaji kuvijua kuhusu kusudi lako. Neema ya Mungu ni kama mwalimu anayekufundisha ili ufaulu mtihani, ndivyo Neema ya Mungu ilivyo. Angalia kwenye Biblia; Tito 2:11-12 .Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa’ Nataka uone hili neno 'nayo inatufundisha'. Neema ya Mungu inapokuja inakuja kukupa maelezo, au kukufundisha kitu gani cha kufanya. Hapo alikuwa anaongelea Neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu, ambayo inatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia, n.k. Lakini linapokuja swala la Neema ya Mungu kwa ajili ya kusudi la Mungu duniani uwe na uhakika itakufundisha pia namna ya kuishi na kutembea kwenye kusudi la Mungu. Sasa unaweza ukaelewa kwa nini nimesema neema ya Mungu inakufundisha na kukuonyesha njia ya kuishi kwenye kusudi la Mungu. Mungu anapotaka kukupa Neema anakupa na maelekezo au mafundisho ili hiyo neema ikufundishe. Najua utaniuliza, atanipaje maelekezo na nitajuaje kuwa haya ndio maelezo ya neema ya Mungu? Ni rahisi sana, Mungu anakupa maelekezo ya Neema kupitia kitu kinachoitwa 'neno la Neema'. Angalia kwenye Biblia uone jambo. Matendo ya Mitume 20:32 ..Basi, sasa nawaweka katika mikono ya Mungu, na kwa neno la neema yake, ambalo laweza kuwajenga na kuwapa urithi pamoja nao wote waliotakaswa. Biblia inazungumzia 'neno la Neema' Na mojawapo ya kazi ya hili 'neno la neema' ni kutujenga na kutupa urithi wa Rohoni. Maana yake Neno la Neema linapoachiliwa kwenye maisha yetu linabeba maelekezo ya kutujenga katika kusudi la Mungu na kutupa urithi wa Rohoni. Neno la Neema ni kama lile alilolipokea Mariamu alipokuwa anapewa ujumbe wa kumpata Yesu kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Lilimsaidia kupambana na makwazo yote yaliyoinuka na kupinga kuzaliwa na kukua kwa Yesu. Mungu anakupa Neno la Neema kupitia Neno Lake Takatifu. Ndio maana ni muhimu sana kusikia Neno la Mungu kila linapokuja. Na ni vizuri zaidi kujifunza kuisikia sauti ya Mungu kwenye maisha yako kwa sababu inakupa maelekezo yote sawa sawaa na neema ya Mungu iliyo juu yako. Nakufundisha hili somo ili uweze kuomba na kutambua ni neema gani uliyonayo, na kuomba Mungu akusaidie kulitambua Neno la Neema kwenye maisha yako. Hakuna Muujiza mwingine wa kuijua neema ya Mungu na neno la Neema ya Mungu kama mahusiano yako na Mungu ni mabaya na kama hutajiingiza kwenye maombi ya kuomba juu ya Neema ya Mungu. INAENDELEA SEHEMU YA PILI